
RAPA Stevo Simple Boy ni msanii mwenye furaha baada ya kampuni moja ya kuuza magari humu nchini kumpa zawadi ya gari jipya.
Msanii huyo ambaye alianza maisha ya kuhangaika katika mitaa
ya mabanda ya Kibera sasa ni mmiliki mpya wa gari aina ya Mazda Demio katika
jiji la Nairobi.
Stevo Simple Boy alivunja taarifa hizi kupitia ukurasa wake
wa Instagram ambapo alionyesha picha kadhaa akiwa amepiga magoti na kusujudu
kando na gari hilo lenye rangi ya divai.
Katika picha nyingine, Stevo Simple Boy alionekana akiwa
amelilalia gari hilo kama anayetaka kulikumbatia kwa furaha na kushukuru
kampuni hiyo na mmiliki wake kwa neema hiyo ya ajabu.
“Asante
@khushimotorskenya kwa zawadi, asante boss @wakasgondal kwa neema, MUNGU
akubariki,” Stevo alichapisha.
Msanii huyo ambaye katika sehemu kubwa ya mwishoni mwa mwaka
jana na mapema mwaka huu amekuwa akifanya vizuri katika vitimbi vyake
mitandaoni amejizolea umaarufu usio na kifani.
Mwishoni mwa mwaka jana, Stevo alikamilisha ziara yake kwenda
nchini Tanzania, katika kile ambacho alikitaja kuwa alikuwa katika mishe za
kufuatilia kolabo yake na bosi wa lebo ya Konde Gang, Harmonize.
Hata hivyo, licha ya kutofanikiwa kukutana naye, Stevo
alisema kwamba mwaka huu hilo litakuwa moja ya ajenda zake kuu kuhakikisha
wanafanikisha kolabo na mkali huyo wa zamani kutoka lebo ya WCB Wasafi.
Bila shaka kupata gari ni hatua kubwa kwa juhudi zake
kimuziki na wengi wanahisi meneja wake mpya, Machabe amekuwa moja kati ya
mihimili ya kumfanikishia Simple Boy ndoto zake, haswa baada ya wengi kudhani
nyota yake ingedidimia baada ya kufeli mikononi mwa mameneji wawili wa awali.