
MTUMIZI mmoja wa mitandao wa TikTok kutoka nchini Indonesia amehukumiwa kifungo cha karibia miaka 3 jela baada ya kupatikana na hatia ya kudhihaki Yesu Kristo.
Ratu Thalisa, Muislamu aliyebadili jinsia alishatkiwa kwa
kosa la kuzungumza na picha ya Yesu kwenye simu yake huku akimtaka kunyoa
nywele zake katika video ya TikTok Live aliyorekodi.
Siku ya Jumatatu, mahakama ya Medan, Sumatra ilimpata
Thalisa na hatia ya kueneza chuki chini ya sheria tata ya matamshi ya chuki
mtandaoni, na kumhukumu kifungo cha miaka miwili na miezi 10 jela.
Mahakama ilisema maoni yake yanaweza kuvuruga
"utaratibu wa umma" na "maelewano ya kidini" katika jamii,
na ikamshtaki kwa kukufuru.
Uamuzi huo wa mahakama ulikuja baada ya makundi mengi ya
Kikristo kuwasilisha malalamishi ya polisi dhidi ya Bi Thalisa kwa kukufuru.
Hukumu hiyo imelaaniwa na mashirika ya kutetea haki za
binadamu likiwemo shirika la Amnesty International ambalo limeeleza kuwa ni
shambulio la kushangaza dhidi ya uhuru wa kujieleza wa Ratu Thalisa na kutaka
ifutiliwe mbali.
"Mamlaka ya Indonesia haipaswi kutumia sheria ya nchi hiyo ya
Habari na Miamala ya Kielektroniki (EIT) kuwaadhibu watu kwa maoni yaliyotolewa
kwenye mitandao ya kijamii," Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty
International Indonesia Usman Hamid alisema katika taarifa yake jinsi
ilivyonukuliwa na BBC.
"Wakati Indonesia inapaswa kupiga marufuku utetezi wa chuki ya
kidini ambayo inajumuisha uchochezi wa ubaguzi, uhasama au vurugu, kitendo cha
hotuba ya Ratu Thalisa hakifikii kizingiti hicho."
Bw Hamid alitoa wito kwa mamlaka ya Indonesia kubatilisha hukumu
ya Bi Thalisa na kuhakikisha kuwa anaachiliwa mara moja kutoka kizuizini.
Pia aliwataka kufuta au kufanya marekebisho makubwa kwa kile
alichokitaja kuwa "vifungu vyenye matatizo" katika Sheria ya EIT -
yaani, wale wanaofanya uhalifu unaodaiwa kuwa wa uasherati, kashfa na matamshi
ya chuki.
Ilianzishwa mwaka wa 2008 na kurekebishwa mwaka wa 2016 ili
kushughulikia udhalilishaji mtandaoni, Sheria ya EIT iliundwa ili kulinda haki
za watu binafsi katika nafasi za mtandaoni.
Imekosolewa vikali, hata hivyo, na makundi ya haki, makundi
ya waandishi wa habari na wataalam wa sheria, ambao kwa muda mrefu wameibua
wasiwasi kuhusu tishio la sheria kwa uhuru wa kujieleza.
Takriban watu 560 walishtakiwa kwa madai ya ukiukaji wa
Sheria ya EIT walipokuwa wakitumia uhuru wao wa kujieleza kati ya 2019 na 2024,
na 421 walitiwa hatiani, kulingana na data kutoka Amnesty International.