
MKEREKETWA wa siasa za upinzani Nuru Okanga amesisitiza kwamba yeye bado ni mwanafunzi licha ya kutoonekana akihudhuria masomo shuleni.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio humu
nchini, Okanga alikanusha madai kwamba anawachezea shere wafuasi wake
mitandaoni kwa kujiita mwanafunzi na kusema kwamba safari yake ya masomo
inaendelea.
Mwanasiasa huyo chipukizi alichangiwa na marafiki zake takribani
miaka miwili iliyopita akisema anaenda shule wakati huo akidai kufanya mtihani
wa darasa la nane, KCPE.
Katika mahojiano hayo, Okanga alisema kwa sasa yuko katika
kidato cha pili na kwamba vipindi vyake vya masomo yeye huvifanya kupitia mitandao.
Alieleza kwamba nyumbani kwake ako na kompyuta ya kipekee
inayomwezesha kuhudhuria vipindi vya masomo kupitia njia ya mitandaoni na
vikiisha anajikita katika masuala mengine.
“Unajua maisha ya leo ni
dijitali. Watu wengi wanasoma online, hata juzi mliona rafiki yangu Oscar Sudi
alipewa cheti na hakuwa anaonekana akienda shule.”
“Sasa hivi vitu vimeingie
kidijitali, tunaingia online kama kuna somo tunasoma hapo ukimaliza unafunga
ukurasa. Mimi kwangu niko na kompyuta, nikijua leo saa Fulani niko na somo Fulani,
nitakaa chini nifungue kompyuta yangu nisome na nikisha maliza, nafunga,” Okanga alieleza.
Alisema kwamba hayo yote japo yanaonekana kama hekaya za abunuwasi
lakini ni mafunzo ambayo yanafanyika katika shule za sekondari Kenya – kwamba mwanafunzi
anaweza soma online.
Mwanasiasa huyo anayesemekana kulenga kiti cha MCA katika
wadi moja kaunti ya Kakamega hata hivyo alikanusha kwamba kwenda kwake shuleni
si kutilia manani ili kuwa na akili bali ameenda kutafuta cheti.
“Hayo yanafanyika
sekondari hapa Kenya. Niko kidato cha pili. Unajua watu wengi wanaona yale
mambo ninaongea ni porojo, lakini kile ninaweza ambia watu ni kwamba sijaenda
kwa shule kutilia maanani, kukuwa na akili. Mimi tayari nina akili. Nimeenda pale
kutafuta vyeti kwa sababu sitaki kuwa MCA pekee yake, nataka nipande ngazi hadi
kuwa MP, gavana na hata rais wa hii nchi,” alibainisha wazi malengo
yake.