

JENERALI mkuu wa majeshi ya Uganda UPDF, Muhoozi Kainerugaba ameanzisha tena upya vita vyake vya mtandaoni dhidi ya msanii mkwasi kutoka Marekani, Jay-Z.
Mwanawe rais Yoweri Museveni sasa
ameibuka na madai mapya kwamba msanii huyo bilionea hakustahili kuwa na
mwanamke kama Beyonce, akisisitiza kwamba mrembo huyo ni wake.
Kupitia ukurasa wake wa X, Muhoozi
Kainerugaba amedai kwamba hata kama Jay-Z ni bilionea – hadhi aliyoitaja kwamba
kwake ni mzaha – utajiri huo wake hauwezi hata kidogo kulinganishwa na mifugo
wake.
Muhoozi alihoji ni kwa nini hajapata jibu
kutoka kwa Jay-Z, wiki chache baada ya kumtaka kukubali pambano ambalo lingeona
mshindi kati yao akimchukua Beyonce kama mke wake – bila kujali kwamba Beyonce
tayari ni mke halali wa bilionea Jay-Z.
Alisema kwamba ikiwa Jay-Z hatatoa tamko,
huenda akapendelea kupanga njama ya kumteka nyara Beyonce na kumchukua kwa
nguvu kutoka kwa Jay-Z.
“Nimesubiri kwa wiki moja sasa.
Hakuna jibu kutoka kwa Jay-Z? Je, niende tu kumkamata huyo mwanamke? Eti Jay-Z ni
bilionea? Huo ni utani! Ng'ombe wangu wana thamani kuliko yeye!”
Muhoozi alihoji.
Mwanajeshi huyo ambaye ameonekana kudata
katika penzi la Beyonce – mama wa Watoto 3 ambaye amedumu kwa ndoa na Jay-Z
tangu 2008 – alisema kwamba wazo la kumkamata kwa nguvu likishindikana,
atakusanya kura ya maoni kuona wangapi wanamuunga mkono kwamba Beyonce anafaa
kuwa wa kwake na wala si wa Jay-Z.
Pia alisema kwamba tangu aanzishe
vuguvugu la kumtaka Beyonce kumwacha Jay-Z na kuja kwake, amepokea mialiko
kadhaa kutoka kwa vyombo vya Habari Marekani vikimtaka kulizungumzia hilo moja
kwa moja kwenye kamera.
“Waafrika na Waasia wangapi
wananiunga mkono katika kumwokoa Beyonce kutoka kwa Jay-Z? Retweet na like. Baadhi
ya Chaneli za Habari za Marekani zimeniomba nije kueleza jinsi Beyonce ni mke
wangu, niko tayari kuja...” Muhoozi
Kainerugaba alisema.
Lakini je, ni kweli kwamba utajiri wa ng’ombe
wa mwanawe Museveni unazidi maradufu utajiri wa msanii Jay-Z kutoka Marekani?
Kwa mujibu wa ripoti ya Forbes ya mwaka
2024, Jay-Z ndiye msanii Tajiri zaidi duniani akiongoza kwa utajiri wa dola
bilioni 2.5 – sawa na shilingi bilioni 323 za Kenya.
Kazi kwako Jenerali Muhoozi Kainerugaba!