
AFISA anayesimamia usafi wa mazingira katika kaunti ya Nairobi, Geoffrey Mosiria ametoa onyo kali kwa hulka ya wachuuzi kuwashambulia na kuwaumiza maafisa wa kaunti maarufu kama kanjo, baada ya mmoja wao kushambuliwa.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mosiria alisimulia jinsi
afisa wa kanjo wa kike alivyoshambuliwa na mtu anayedaiwa kuwa mchuuzi katika
moja ya mitaa ya katikati ya Nairobi.
“Ni jambo la kusikitisha
sana na halikubaliki kabisa kwamba mchuuzi alichagua kumshambulia afisa wa
kaunti (mwanamke Askari wa kaunti) ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake
halali akiwaomba waondoke kwenye njia ya umma ili kuruhusu watembea kwa miguu
bila malipo. Hiki ni kitendo cha kutokujali cha hali ya juu, na hatutaruhusu
kiende bila kuadhibiwa. Hatutaogopa. Utaratibu lazima udumishwe, na utawala wa
sheria lazima itawala,” Mosiria alitema cheche.
Kwa mujibu wa Mosiria, wachuuzi huwa hawalipi kodi yoyote kwa
serikali ya kaunti ya Nairobi na waliruhusiwa kuendesha biashara zao katika Maeneo
waliyotengewa kwa hisani ya gavana lakini sasa wameanza kutumia vibaya ruhusa
hiyo.
“Wachuuzi jijini Nairobi hawalipi ada yoyote
kwa serikali ya kaunti. Kwa nia njema, Mheshimiwa Gavana amewaruhusu kufanya
kazi kutoka kwa njia maalum za nyuma ili kukuza fursa jumuishi za kiuchumi.
Hata hivyo, wengine sasa wanatumia vibaya fursa hii kwa kuvamia njia za kupita
miguu, kuzuia watembea kwa miguu, na mbaya zaidi kutumia vurugu wanapotakiwa
kuzingatia sheria,” alifafanua.
Afisa huyo wa mazingira aliapa kwamba uongozi mzima wa kaunti
utahakikisha mchuuzi aliyetekeleza kitendo hicho kwa mwenzao anachukuliwa hatua
madhubuti.
“Ifahamike wazi: afisa
huyu ni binti wa mtu, mama wa mtu, na mtumishi wa umma aliyejitolea kutumikia
watu wa Nairobi. Shambulio lolote dhidi ya afisa mmoja wa kaunti ni shambulio
dhidi ya wafanyikazi wote wa kaunti, na tutajibu kwa uthabiti.”
“Hatutavumilia uasi. Watu
waliohusika katika shambulio hili watatambuliwa, kukamatwa, na kufunguliwa
mashtaka kwa kiwango kamili cha sheria. Pia tunakagua itifaki za utekelezaji
ili kuhakikisha usalama na utu wa maafisa wetu wote wanaosonga mbele,” aliapa.
Katika siku za nyuma, vilio vilivyokuwepo ni vya maafisa wa
kaunti kushambulia wachuuzi na hata kuharibu mtaji wao.