Takriban wiki mbili tu baada ya kuthibitisha mwisho wa uhusiano wake wa miaka mitatu na muigizaji Tyler Mbaya almaarufu Baha, mtayarishaji wa maudhui Georgina Njenga ameshiriki ujumbe wa kimafumbo ambao umezua gumzo mitandaoni.
Siku ya Jumanne, mama wa binti mmoja kupitia ukurasa wake wa Instagram alishiriki video ya tiktok yenye nukuu ya kejeli ya jinsi wanaume wanavyofanya baada ya mahusiano kufika mwisho.
Chapisho hilo lilizungumzia jinsi baada ya mahusiano kuisha, wanaume huwa wanadai walikuwa na mipango mikubwa na wapenzi wao kabla ya kuachana nao.
“When you stop dating him, that is when you will hear “I had so many plans for us but you messed up” Okay Mr event planner we hear you,” maelezo ya video hiyo yalisomeka.
Kumaanisha: "Unapoachana naye, hapo ndipo utasikia "Nilikuwa na mipango mingi kwa ajili yetu lakini umevuruga" Sawa Bwana mpangaji wa hafla tunakusikia."
Chapisho la Georgina linakuja wiki mbili tu baada ya kuthibitisha kwamba hachumbiani tena na muigizaji huyo wa zamani wa kipindi cha Machachari kwenye runinga ya Citizen TV.
Katikati ya mwezi huu, mama wa mtoto mmoja msichana alithibitisha kuachana na Baha baada ya kuulizwa iwapo bado yuko na muigizaji huyo katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye Instagram.
"Je wewe na Tyler Mbaya bado wako pamoja?" Shabiki mmoja alimuuliza Georgina.
Ambapo alijibu; "Hapana! Tuliachana.”
Mtumizi mwingine wa Instagram aliuliza swali hilo hilo, huku akitaka kujua ikiwa mtayarishaji huyo wa maudhui bado ana uhusiano mzuri na Baha ambaye alidai kuwa hivi sasa tayari yuko kwenye uhusiano mpya.
“Kwa wasiwasi tu, mko sawa na Baha?”aliuliza shabiki.
Georgina akajibu; "Wengi wenu mnauliza swali hili. Hii ni mara ya mwisho nitajibu. Tuliachana na niko kwenye uhusiano mpya na mwanaume wangu mpya,”.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa wapenzi hao kudokeza kuwa wameachana.
Wiki chache kabla, Baha alikuwa amedaiwa kuwa mlaghai, tukio ambalo linasemekana kutikisa uhusiano wake na Georgina.
Zaidi, miezi michache iliyopita, Georgina aliuambia ulimwengu kuwa hakuwa tena na uhusiano wa kimapenzi na Baha lakini baadaye alibadili kauli yake akisema ulikuwa ni mchezo tu.