Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah hatimaye amefichua ni kwa nini alitoa taarifa ya kumkana binti yake na mpenzi wake wa zamani, Caroline Muthoni.
Akiongea kwenye video iliyochapishwa kwenye chaneli ya YouTube ya Ruth K, mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alidai kwamba alichukua hatua hiyo kutokana na shinikizo kubwa lililokuwa likiendelea maishani mwake.
Alisema shinikizo lilianza kuongezeka kufuatia posti za mzazi mwenzake na mahojiano ambayo alifanya baada ya wao kutoa habari kuhusu kutengana kwao.
“Nilianza kukasirika, nikaanza kujibu kwa kupost vitu ambavyo sitakiwi kupost. Ninaamini Mungu kwamba alinishikilia, sikuposti kila kitu. Nimeshikilia vitu vingi sana ambavyo vikisemwa, vitaathiri vibaya maisha ya watu wengine, au vitachukuliwa vibaya," Mulamwah alisema.
Baba huyo wa watoto watatu alidai kuwa alitaka kuwafanya watu waache kumhusisha na mambo ambalo mzazi mwenzake alichapisha au kuzungumzia kwenye mahojiano.
“Nilipopost hivyo, nilitaka nibaki kando ya hii story ili wewe (Carrol) ukienda kwenye mahojiano mengine uongelee kuhusu mtoto wako, nisiwekwe kwa mix. Hilo lilikuwa wazo langu, baada ya hapo mambo ikaanza kuwa mingi,” alisema.
Mulamwah alibainisha kuwa matukio yaliyofuata baada ya chapisho lake hata hivyo hayakuwa sawa kwani yeye na Carrol walikabiliana na unyanyasaji mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mtoto wao.
Hata hivyo, mchekeshaji huyo aliweka wazi kuwa anafurahi kwamba alichukua hatua hiyo kwani lilikuwa chaguo bora zaidi, kwani shinikizo lilimfanya afikirie kufanya mambo mengine mabaya zaidi.
"Ilinibidi nichague kubaki hai kwangu. Ndio maana nililazimika kusema kwamba huyu sio mtoto wangu. Ili msinihukumu kulingana na hilo kwa sababu shinikizo lilikuwa linaongezeka. Ilikuwa shinikizo nyingi, mbaya sana.
Hiyo ndiyo njia pekee kwa nini ninaishi leo, kwa sababu nilikuwa nikifikiria njia zingine, yaani kutokana na hii stori nilifikiri ninafaa niende mahali na labda nifanye kitu mbaya kwa watu wengi na kwangu. Hayo yalikuwa mawazo yangu,” alisema.
Mnamo Aprili 2022, Mulamwah alishangaza watu wengi alipotangaza hadharani kwamba Keilah, bintiye aliyezaa na Carrol Sonie si mtoto wake.
Haya yalijiri baada ya wiki kadhaa za drama isiyoisha kati yake na mpenzi wake wa zamani kwenye mitandao ya kijamii.