Msanii na mjasiriamali mashuhuri nchini Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amesimulia jinsi alivyonusurika kifo wakati alipokuwa katika mtaa wa Westlands, Nairobi siku ya Jumatano, Januari 22.
Mama huyo wa watoto watano alikuwa kwenye ghorofa ya tatu ya jengo moja kwa ajili ya mazoezi wakati moto uliripotiwa kuzuka katika jengo hilo na watu kuanza kutolewa nje.
Akothee alizungumza kuhusu jinsi matukio yalivyokuwa ya kutisha wakati juhudi za kuwaelekeza watu nje zilikuwa zikiendelea.
“Tukiwa tumechanganyikiwa, tulitoka nje kwa kasi, lakini tukakumbana na moshi mwingi uliojaa kwenye ngazi za kutoroka. Moshi ulikuwa mnene na giza, na hapakuwa na njia nyingine ya kutokea. Mwanzoni, nilibaki mtulivu, nikifikiri tunaweza kushuka kwenye ngazi. Hata hivyo, tulipojaribu, mafusho yalizidi kuongezeka, na tukaanza kukohoa bila kudhibitika. Kisha likaja onyo la kutisha: "Epuka ngazi!", Akothee alisimulia.
"Ikiwa hatungeweza kutumia ngazi, tulipaswa kufanya nini? Hofu ilianza kutanda huku tukikimbia huku na huko, kutafuta njia mbadala. Nje, umati ulisimama, simu zikiwa mkononi, zikiturekodi tulipokuwa tukihangaika. Nikiwa nimeshika mkono wa kaka yangu, nilijitayarisha kwa mabaya zaidi. Nilikuwa na hakika kwamba hatutaishi, "aliongeza.
Mwimbaji huyo alisema kwamba alimtupia mtu
anayemfahamu funguo za gari lake ili gari hilo lipelekwe nyumbani kwake ikiwa
lolote lingetokea.
"Wakati tu yote yalionekana kupotea, usaidizi ulifika. Ngazi ililetwa, nasi tukaelekezwa twende orofa ya pili. Kupanda chini hadi ghorofa ya pili, kupumua kukawa nzito kwa kila hatua. Kwa uharaka, tulipanda kwenye ngazi na kuepuka mafusho makali. Niliposhuka, bado niliona watu wakirekodi tukio hilo, bila kujali woga na kukata tamaa kwetu,” alisimulia.
Mwimbaji huyo alisema kwamba mawazo ya tukio hilo la kutisha yalimkumba sana alipofika nyumbani hivi kwamba alitokwa na machozi.
"Niliangua kilio, nikizidiwa na kufikiria maisha ya watoto wangu na wale wanaonitegemea wangekuwaje nisipokuwepo. Mungu ukifika wakati wa mimi kupumzika usiniache niogope, niache nilale kwa amani bila shida,” alisema.