Mwanasosholaiti na mfanyibiashara maarufu
wa Kenya Faith Makau almaarufu Amber Ray amekiri kuwa amewahi kuolewa kama mke
wa pili mara mbili.
Katika chapisho kwenye Instagram, mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kuwa hakuwahi kujua kuwa wanaume ambao walimuoa kama mke wa pili walikuwa wameoa.
Amber Ray alifichua hayo alipokuwa akiwajibu wakosoaji waliomshtumu kwa kuwa mnafiki na kuharibu ndoa za wanawake wengine.
"Inashangaza jinsi watu wengine wanavyojaza DM yangu kwa matusi kwa sababu tu nilitangaza maoni yangu kuhusu hadithi ya Annie. Nimeitwa mnafiki, nikituhumiwa kuwafanya wanawake wengine kulia kwa sababu nilikuwa mke wa pili,” Amber Ray alisema Jumatatu jioni kupitia Instagram.
Mwanasosholaiti huyo alieleza kuwa wanaume ambao walimuoa kama mke wa pili walimdanganya, na akaangukia kwenye mtego wao bila kujua.
“Ngoja niwakumbushe jambo hili; Nimeshiriki ukweli wangu waziwazi. Ndiyo, niliolewa mara mbili kama mke wa pili, lakini ukweli ni kwamba, sikujua walikuwa wameolewa. Nilidanganywa, nikatumiwa, na kuachwa kubeba lawama zote-lawama nilizochukua kama somo. Nilishiriki hadithi yangu kwenye YouTube kwa sababu ninakataa kuficha maisha yangu ya zamani, "alisema.
Kipusa huyo mrembo alibainisha kuwa hakuwa mpango wa kando wa kwanza au wa mwisho, na akaweka wazi kuwa tayari ameshasonga mbele na maisha yake baada ya makosa ya zamani.
Pia alilalamika kuhusu jinsi jamii inavyowahukumu wanawake kwa ukali wanapolaghai na kuhalalisha vitendo vya wanaume wanapofanya vivyo hivyo.
“Niweke wazi; hakuna mtu anayeweza kunifanya nijisikie vibaya kuhusu maisha yangu ya zamani tena. Nimepona, nimekua, na sipo hapa kubeba aibu ambayo si yangu,” Amber alisema.
"Ikiwa uko kwenye DM zangu na uhasi, okoa nguvu yako- haitanivunja. Kwa wengine wote: hebu tuzingatie kuwawajibisha watu wanaofaa na kusaidiana kukua na kuponya!” aliongeza.