
Mwanzilishi wa Kanisa la Neno Evangelism Centre, Mchungaji James Maina Ng’ang’a, alipata nafasi nyingine ya kukutana tena na mwanaume aliyezaba makofi katika tukio lililonaswa kwenye video iliyosambaa sana mtandaoni.
Katika ibada ya hivi majuzi kanisani mwake jijini Nairobi, mhubiri huyo mashuhuri na anayezingirwa na utata mwingi alimuita mwanaume huyo asimame mbele ya kanisa wakati akiendelea na mahubiri yake.
Mwanaume huyo alipofika madhabahuni, Ng’ang’a alichukua fursa hiyo kuelezea jinsi muumini huyo aliwahi kumfikia kwa simuawali na jinsi alivyomkaribisha kuhudhuria ibada ya kanisani mwake.
Wakati akihojiwa, mwanaume huyo ambaye alikuwa amevalia shati jekundu na suti ya kijivu alithibitisha kuwa ndiye aliyepokea makofi mawili kutoka kwa mchungaji huyo na hata kusema yuko tayari kupokea kofi jingine.
“Haina shida. Iko sawa. Mradi nipone na injili iendelee,” alisema mwanaume huyo ambaye hakutaja jina lake.
Muumini huyo aliendelea kueleza kuwa yuko tayari kutumika kama mfano kwa wengine wanaolala wakati wa ibada.
“Nataka niwe mfano kwa wengine. Huwezi kaa na mapepo ndani yako ama kizuizi, Mungu hawezi kuja ndani yako. Hiyo makofi ni nzuri juu ni ya baraka,” aliongeza.
Huku akieleza kuhusu matatizo yaliyomfanya atafute maombi kutoka kwa Mhubiri Ng’ang’a, mwanaume huyo alisema alikuwa akipata ndoto mbaya ambazo haziwahi kuisha licha ya kufunga na kuomba milimani.
Alisema kuwa alikuwa akihangaika na ndoto zinazohusisha mke wa kiroho, lakini mhubiri huyo alimwombea wiki chache zilizopita na akampiga tena kofi, jambo lililomfanya ajisikie huru.
“Sasa umenipiga makofi mara mbili. Hiyo haikuonekana. Nilianguka chini ukaniombea nikaskia niko huru,” alisema.
Mwanaume huyo alisema hajui ni kwa nini alilala wakati wa ibada ya Ijumaa iliyopita, hali iliyomfanya mchungaji Ng’ang’a ampige tena.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kwa kawaida yeye huwasili kanisani mapema.
“Mimi nikikuja nilikuja nasubiri neno. Ata sijui mahali usingizi ilitoka. Sijui,” alieleza.
Baada
ya kumtambulisha kwa waumini wake, Mchungaji Ng’ang’a alisema: “Ukipenda mtoto
unamchapa. Even my Master, my Lord, alikuta watu wakiuza kwa hekalu, akapindua
meza zao na akawachapa.”