Otile Brown afunguka kuhusu maisha ya muziki na mahusiano na wanadada

Otile amesema yupo single na hayupo kwenye harakati za kutafuta mchumba.

Muhtasari

•Otile amefichua kuwa safari yake ya muziki iling'oa nanga zaidi ya mwongo mmoja uliopita wakati bado  akikua katika kaunti ya Mombasa.

•Amebainisha kuwa huwa anaimba kutokana mapenzi tupu na matarajio yake ni kuhamasisha watu kupitia nyimbo zake.

•Amedai kuwa utafutaji wa mpenzi umekuwa kizungumkuti kwake katika nafasi aliyopo kwa sasa na hivyo anachukua muda wake.

katika studio za Radio Jambo mnamo Julai 15, 2022
Msanii Otile Brown katika studio za Radio Jambo mnamo Julai 15, 2022
Image: RADIO JAMBO

Staa wa Swahili RnB Jacob Juma Obunga almaarufu Otile Brown amefunguka kuhusu kazi yake ya muziki na mahusiano yake.

Otile amefichua kuwa safari yake ya muziki iling'oa nanga zaidi ya mwongo mmoja uliopita alipokuwa akiishi Mombasa.

"Mwaka wa 2012 tulikuwa tunaimba mtaani, lakini kile kiwango cha kiutani utani. Mimi nilifikia mahali nikaanza kutumbuiza maana nilipenda muziki nikiwa mdogo sana," Otile alisema katika mahojiano ya hivi majuzi na Radio Jambo.

Mwanamziki huyo mwenye umri wa miaka 30 alifichua kuwa ndoto yake kubwa tangu utotoni ilikuwa kufanya muziki, jambo ambalo lilimsukuma kugura Mombasa na kuhamia Nairobi katika juhudi za kuifanikisha ndoto yake.

"Nairobi yenyewe ilikuwa sijui mtu, nilitafuta rafiki wa kitambo ambaye nilikuwa namjua. Hakuwa kutoka Mombasa, alikuwa wa Kisumu. Nilipokuja Nairobi nikakaa naye kidogo na nikaanza kufanya biashara," Alisimulia.

Otile alifichua kwamba mwanzoni alijiunga na uigizaji akiwa na matumaini ya kupata njia ya kufanikisha ndoto yake ya muziki. 

Wakati akifanya kazi katika sekta ya uigizaji  aliweza kukutana na watu waliomsaidia kujitosa kwenye sanaa ya muziki. Kutoka hapo alianza kupiga hatua moja baada ya nyingine hadi kufikia kiwango cha kutambulika nchini.

Mwanamuziki huyo alikiri kuwa alifurahi sana kuona wimbo wake ukichezwa kwenye runinga kwa mara ya kwanza.

"Siku moja DJ Pinye alicheza wimbo wangu 'Imaginary Love' ambao tulikuwa tumefanya na Khaligraph. Wakati huo pia yeye alikuwa msanii chipukizi tu. Tulikuwa tumeanza tu lakini wimbo ulikuwa mzuri. Tukiwa mtaani nilishangaa wimbo umechezwa kwa The Beat kwa mara ya kwanza. Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya furaha zaidi maishani. Nilifurahi sana," Alisema.

Otile  alieleza kuwa ilimchukua miaka mingi kukubalika na kujizolea umaarufu mkubwa alio nao kwa sasa. Alisema alianza kukubalika takriban miaka mitano iliyopita baada ya kuachilia kibao 'Alivyonipenda' ambacho alimshirikisha King Kaka.

Otile pia alibainisha kuwa huwa anaimba kutokana na mapenzi  na matarajio yake ni kuhamasisha watu kupitia nyimbo zake.

"Napenda nifocus na muziki wangu. Sitaki nijulikane kwa matukio. Nikijulikana kwa kiki na kuvuma ina maana nitafanya hizo kiki milele. Hilo huzeeka," Alisema.

Katika mahojiano hayo, staa huyo wa muziki pia alifunguka kuhusu masuala kadhaa yanayohusu mahusiano yake.

Alifichua kuwa kwa sasa yupo single na kubainisha kuwa hata hayupo kwenye harakati za kutafuta mchumba.

"Nipo single saa hii. Nachukuwa muda wangu. Ni ngumu kwangu. Mimi kuwa katika nafasi hii kwa sasa siwezi kujua ambaye ninakutana naye kama ni mkweli au la," Alisema.

Otile alidai kuwa shughuli ya kumsaka mpenzi imekuwa kizungumkuti kwake katika nafasi aliyopo kwa sasa na hivyo anachukua muda wake.

Huku akifafanua zaidi alisema kuwa mahusiano yake ya awali  yalimfanya kuwa mwangalifu zaidi katika ulingo wa mahaba.

"Kila mtu ambaye anakuja inakuwa lazima namhakiki. Ni kama unawaangalia kweli anaweza ama hawezi. Labda utakuta kuna vitu amefanya, unaona huyo sio yeye. Ni mtihani mkubwa," Alisema.

Gwiji huyo wa muziki pia alieleza kuwa haijakuwa rahisi kwake kutowafautisha watu wanaoukuja katika maisha yake na nia nzuri na wale wanaokuja na malengo mabaya.

Licha ya kuwa kwa sasa hatafuti mchumba, Otile alibainisha kuwa hatasita kujitosa kwenye mahusiano ikiwa mrembo mwenye hulka anazotaka atajitokeza.

"Sitafuti kabisa. Nachukua muda wangu. Nataka awe ametumwa kwenye njia yangu. Huwezi kutafuta mwenzi wako. Ni ngumu sana,"

Aidha alishauri kuwa wakati mzuri wa kupata mchumba ni wakati ambapo mtu anajijenga wala sio baada ya kufanikiwa.

Sio mahusiano mengi ya zamani ya Otile ambayo yanajulikana hadharani. Wapenzi wake wa zamani ambao wanajulikana ni mwanasosholaiti Vera Sidika na mwanamitindo Nabayet almaarufu Nabbi.

Mwanamuziki huyo  na Vera walitengana mwaka wa 2018 baada ya kuchumbiana kwa kipindi kifupi. Utengano wao ulijaa tope huku wawili hao wakianikana hadharani kuhusu mambo mbalimbali ya chumbani.

Baada ya kutengana na mwanasosholaiti huyo haikuchukua muda mrefu kwa moyo wa Otile kutekwa na malkia mrembo kweli kutoka Ethiopia, Nabayet.

Otile alikuwa na mahusiano mazuri ya umbali na kipusa huyo wa Ethiopia kwa takriban miaka mitatu kabla ya kutengana.

Mwanamuziki huyo alitangaza habari za kutengana na Nabbi mapema mwaka huu baada yao  kushindwa jinsi ya kuendeleza mahusiano yao ya simu.

"Mimi na Nabbi hatuko pamoja tena. Mara ya mwisho tulikuwa pamoja ilikuwa kujaribu kutafuta njia ya mbele lakini tuliamua kwenda tofauti kwa bahati mbaya," Otile alitangaza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Otile alimtaja mpenzi huyo wake wa zamani kama mtu mzuri ambaye angeendelea kuheshimu na kujali licha ya kutengana.

"Yeye ni mtu mzuri na kwa hilo, nitamheshimu kila wakati, nitamjali na kuwa uhusiano mzuri naye. Namtakia mafanikio mema ya kusonga mbele,” Alisema.

Siku chache zilizopita mwanamuziki huyo alikiri upendo wake kwa mwimbaji wa R&B Toni Braxton.

Otile alieleza hisia zake kwa mwanamuziki huyo wa Marekani kwenye Instagram na  kumtambua kama kiumbe maalum cha Mungu.

"Bado namcrushia.. Mmoja wa wanawake wazuri zaidi ambao Mungu aliwahi kuumba," Otile aliandika.

Tangu kutengana kwake na Nabayet miezi kadhaa iliyopita, Otile hajatambulisha wala kuonekana na mpenzi mpya. Badala yake ameonekana kuondoa fikra zake zote  kwa mahusiano na kuziweka zote kwenye muziki.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO.