Meneja wa msanii Diamond Platnumz Babu Tale amepakia msururu wa picha akimsuka bintiye nyewel na kudai kuwa hakuna kitu kinampa furaha na faraja ya moyoni kama kulea watoto wa kike.
Tale alionekana ameketi kwenye mkeka na binti yake akimfanyia utaalamu wa kichwani kuweka nywele sawa na kufichua kwamba ana uhusiano mzuri sana tena wa karibu baina yake na watoto wake wa kike.
“Leo bint kaniomba nimsuke na mimi sijui hata pakuanzia,” Babu Tale alisema.
Hata hivyo, Tale alifunguka kuwa kuna changamoto kwani bintiye ni raha kumlea akiwa mdogo lakini huku mbeleni kadri umri unavyozidi kusonga kutatokea mambo mengine yatakayozua ukakasi.
Tale kwa mfano alisema kuwa bintiye hamfichi kitu chochote na anashangaa itakuwaje akiwa mtu mzima na apate mpenzi halafu aje kumvunja moyo atalazimika kulia na yeye.
“Ulezi wa mtoto wa kike utotoni unaraha sana ila kila anavyozidi kusogea nahisi changamoto maana kila kitu ananiambia mimi sasa uko mbele sijui itakuaje akitokea mpuuzi wa kumuumiza moyo sijui na mimi nitaumia kama yeye,” Tale aliandika.
Mashabiki walimfurahia tale kwa kulea watoto wake bila kuoa mke mwingine tangu kifo cha mke wake.
“Kama umeweza kukaa hadi chini na kunyoosha miguu. Una kitu Babu Tale, utafika mbali,” mmoja aliwambia.
“Kama uliwaumiza watoto wa watu naye lazima ataumizwa, lakin kama hukufanya hivyo shaka ondoa. Maana imeandikwa kama utavyo fanya ndivyo utavyofanyiwa,” mwingine alisema.