Msanii wa Bongo Fleva, Mbosso Khan kwa mara ya kwanza amesimulia jinsi kutokuwa na elimu ya Kiingereza kulimjengea mazingira magumu akiwa katika ziara yake ya kimuziki nchini Ujerumani.
Akizungumza na blogu ya Simulizi na Sauti, Mbosso alisema kwamba anakumbuka jinsi alitaabika kiasi kwamba alimpa kazi ngumu sana meneja wake.
Msanii huyo alisimulia kwamba kila kitu alichokuwa anaulizwa kwenye mahojiano, alikuwa anasikia neno la mwisho tu asijue cha kujibu.
“Nakumbuka mara ya kwanza nilipoenda Ujerumani mwaka 2019, kipindi kile meneja wangu Sandra Brown alipitia kipindi kigumu sana, yaani nilikuwa naulizwa swali nasikia neno la mwisho tu. Yaani anaongea unasikia neno la mwisho, unajua,” alisema.
Hata hivyo, msanii huyo wa WCB Wasafi alifunguka kwamba kwa sasa anajitahidi kabisa kutenga muda kujifunza baadhi ya maneno ya msingi ya Kiingereza tofauti na mwanzo.
“Najitahidi kama kipindi hiki najifunza tofauti na mwanzo. Najaribu sana,” aliongeza.
Msanii huyo pia alifunguka kwamba kaitka kolabo yake na marehemu Costa Titch kutoka Afrika Kusini, kuna baadhi ya mistari ya Costa Titch kwenye kolabo yao ambao mpaka sasa hivi hawezi kuiimba kutokana na kutokuwa na elimu ya Kiingereza.
“Kuna kipindi nakumbuka nilitoa wimbo na marehemu Costa [Titch], nafikiri ‘Moyo’ mimi vesi ya marehemu siwezi kuimba mpaka leo. Siwezi na sidanganyi, sijashika maneno nateseka kabisa kwa sababu mimi sina elimu ya kiingereza,” alifichua.
Mbosso alisema kwamba kwa asilimia kubwa anahisi kutokuwa na ujuzi wa Kiingereza na kielimu kumemfungia baadhi ya fursa nzuri, akisema kwamba yeye leo hii akiketi kwenye baraza lolote atasisitiza tu watu wasome.
“Elimu bwana sio shule tu, yaani kwenye kila angle yaani mimi nikikaa sehemu yoyote tu nitasema watu wasome. Hata kama una talanta kiasi gani ila ukiwa na ufinyu wa lugha, kuna baadhi ya sehemu unashindwa kuingia vizuri,” Mbosso alishauri.