
Msanii maarufu wa muziki wa bongo nchini Tanzania Diamond Platinumz amewahimiza Waislamu wenzake kusuali sana mbali na kufunga mwezi huu mtukufu wa ramadhani.
Diamond akizungumza kwa njia video kupitia ukurasa wa Wasafi aliwataka watu kuwa na umoja na kuonesha imani kwa wengine msimu huu wa mwezi mtukufu.
"Mungu ni mwema wakati huu, muda usiokuwa mrefu naingia kuswali na kufuturu, msifunge tu ila msali. Hakikisha unafunga na unaswali itampendeza mwenyezi Mungu," alisema Diamond akionesha kuelekea msikitini.
Msani huyo ambaye aliweka video mbili tofauti, moja ikiwa kabla ya kuingia msikitini na nyingine akitoka msikitini, aliwataka binadamu kuchagua kutenda mema kwenye video ya pili.
Alisisitiza kwamba wakati huu ni wa muhimu sana kwa waislamu wote na wanapaswa kumushukuru Mungu.Alieleza kwamba hata wale waliobarikiwa kiasi gani ni wakati wa kurejesha shukrani.
"Kutoka saa nane mpaka sasa ivi sa tisa kasoro, tumekuwa msikitini. Hakikisha unafanya mambo ambayo yanampendeza mwenyezi Mungu wakati huu. Sisi kama vijana ambao tuna baraka na tumebarikiwa, lakini wakati kama huu lazima tumushukuru Mungu. Kila mtu autumie vizuri huu mwezi kama alivyotuhimiza, miezi mingine inakuanga vigumu lazima tukubali. Lakini mwenyezi Mungu anatujalia kwa kutuongoza na kutubadilisha kiutaratibu alihamudilahi radhi, Naitwa Naseeb Abdul," alikamilisha ujumbe msani huyo wa Tanzania.
Diamond Platinumz jina lake halisi ni Nasibu Abdul Juma Issaack, pia anajulikana kwa majina Mengi ya Kisanii kama vile Chibu, Simba, Nasibu kichwa, Simba la masimba ama Dangote kwa sasa ana umri wa miaka 35.
Diamond ni mwimbaji na mtunzi wa muziki wa Kitanzania ambaye ana uwezo mkubwa wa kiushindani, hivyo ana mashabiki wengi ndani na nje ya Tanzania. Inasemekana kuwa ndiye msanii wa Afrika Mashariki na Kati anayependwa na kupambwa na watu wengi zaidi kwa sasa.