KIONGOZI wa wengi katika bunge la kitaifa ambaye pia ni mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wah ameteuliwa kuwa ajenti mkuu wa Raila Odinga kwenye uchaguzi wa AUC mwezi ujao.
Haya ni kwa mujibu wa
naibu wa rais Kithure Kindiki ambaye alimtangaza mbunge huo kuwa wakala wa
Odinga wakati kura hizo zitakapopigwa na marais wa bara Afrika.
Akizungumza siku ya Ijumaa,
Kindiki alisema Ichung’wah ataenda Addis Ababa, Ethiopia angalau wiki moja
kabla ya uchaguzi, na atarejea tu nchini baada ya Raila kuapishwa, iwapo
atashinda.
Naibu rais alifichua
kwamba amemtwika Ichung’wah wajibu huo kwa kuwa yeye pia alikesha katika ukumbi
wa Bomas kwa wiki nzima kama ajenti wa William Ruto wakati wa uchaguzi wa urais
Agosti 2022.
“Nilikuwa ajenti mkuu wa
Rais William Ruto kwa siku saba nililala huko (Bomas). Ajenti mkuu wa Raila
Odinga mjini Addis Ababa, Ethiopia atakuwa Kiongozi wa Wengi Kimani
Ichung’wah,” Kindiki alisema.
Naibu Rais alizungumza
wakati wa mkutano na ujumbe wa viongozi waliochaguliwa, wafanyabiashara na jamii
kutoka kaunti ya Kajiado.
Kindiki alibainisha kuwa
iwapo Rais William Ruto na Raila wasingekubaliana kufanya kazi pamoja kwa
manufaa ya nchi, Kenya isingepata fursa ya kutoa mgombea wa kuongoza Tume ya
Umoja wa Afrika.
Alisisitiza kuwa
serikali iko tayari kufanya kila iwezalo kuhakikisha Raila anaibuka mshindi
katika uchaguzi wa AUC.
“Kama Ruto na Waziri
Mkuu Raila wangeendelea na siasa za mgawanyiko za kuwahadaa watu na hakuna
kampeni inayoendelea, Kenya ingepoteza fursa tuliyo nayo sasa. Tutatoka nje ya
njia yetu. Tunamuombea Raila Odinga. Tunafanya kazi kwa bidii, Ruto anamfanyia
kampeni na hatutaacha jambo lolote lile,” akasema.
Raila anakabiliwa na
changamoto kutoka kwa wagombea wengine wawili, akiwemo Mohamoud Youssouf wa
Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar.
Uchaguzi huo utafanyika
Februari 25.
Mshindi wa kiti cha
mwenyekiti wa AUC anatakiwa kupata uungwaji mkono wa thuluthi mbili ya nchi 55
zinazostahili kupiga kura, ikiwa ni tafsiri ya nchi 33 wanachama wa Umoja wa
Afrika.