
IDARA ya upelelezi wa jinai, DCI wamefichua kwamba kurasa zao
kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na X zilidukuliwa japo kwa muda mchache
usiku wa Jumapili, Februari 9.
Sasisho hilo lilichapishwa kwenye ukurasa huo wa X saa chache
baada ya msururu wa machapisho ya kutiliwa shaka kwenye ukurasa huo.
Kwa mujibu wa sasisho hilo, wadukuzi walifanikiwa kuchukua
uthibiti wa akaunti zao kwa muda mfupi na kuanza kuchapisha jumbe za utani.
Hata hivyo, DCI waliweka wazi kwamba walifanikiwa kuzirudisha
akaunti zao mikononi mwao na kuweka wazi kuwa machapisho hayo hayakuwa kutoka
kwa idara hiyo ya upelelezi.
“Kwa muda fulani jioni
hii, tulipata mashambulizi ya mtandaoni kwenye mifumo ya kidijitali ya DCI (X
na Facebook), lakini tangu wakati huo tumepata udhibiti kamili. Katika kipindi
kifupi, wahalifu wa mtandao waliojaribu kuchukua akaunti walichapisha maelezo
yaliyonaswa kwenye picha ya skrini iliyo hapa chini,” DCI walisema kupitia X.
Idara hiyo ambayo imekuwa chini ya ukosoaji mkali kutoka kwa
sehemu ya Wakenya kutokana na msururu wa utekaji nyara iliarifu kwamba
uchunguzi dhidi ya tukio hilo la udukuzi umeanzishwa.
“Kumbuka: Kwa hivyo
habari hiyo ni FEKI na sio kutoka kwa DCI. Uhoji wa kina katika shughuli za
uhalifu umeanzishwa ili kuwaweka rumande wahusika,” walisema.
Udukuzi huu unajiri siku chache baada ya akaunti za X za
mashirika ya habari KBC na K24 kudukuliwa pia.