
Aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka ametoa onyo kali kwa Rais William Ruto, akimwonya dhidi ya kudharau uwezo wa Gen Z katika ushawishi wa kisiasa.
Akizungumza , Kalonzo alihusisha kushindwa kwa Raila Odinga katika uchaguzi uliopita wa Tume ya Umoja wa Afrika kutokana na ushawishi usiotarajiwa wa uanaharakati wa Gen Z, ambao alidai ulichangia pakubwa katika kuchagiza matokeo.
Alisema kuwa wanaharakati vijana waliweza kuhamasisha na kushawishi moja kwa moja watoa maamuzi, jambo ambalo taasisi ya kisiasa haikutarajia kikamilifu.
“Ninaweka lawama kwa Rais William Ruto, ambaye ndiye aliyekuwa mpiga kampeni mkuu. Alikuwa na nia tofauti kwamba labda akimskuma Raila atakuwa na wakati rahisi zaidi, lakini hakujua kuwa itakuwa ngumu sana. Na pia ikumbukwe vijana wa Gen Z wako na uwezo wa kuloby, and they lobbied directly. Hii ndiyo sababu nyingine kuu ya Raila kushindwa,” Kalonzo alisisitiza.
Alifafanua jinsi wanaharakati vijana walihusisha kuwania kwa Raila Odinga na serikali ile ile waliyoshikilia kuwajibika kwa kukandamiza maandamano.
Alisisitiza kuwa bendera ya Kenya iliyobebwa na Raila katika kampeni yake inaashiria utawala ule ule ambao ulishutumiwa kuwaua waandamanaji wasio na silaha, haswa waandamanaji wa Gen Z ambao walikabiliwa na nguvu za kikatili na vyombo vya usalama.
Ghasia zinazoshukiwa kufadhiliwa na serikali dhidi ya wanaharakati vijana, alisema, zilipunguza kwa kiasi kikubwa uungwaji mkono wa kuwania kwa Raila, kwani nchi nyingi zilihusisha mbio zake na utawala unaotawala.
“Wewe, Raila hakuwa Raila; alikuwa mgombea wa Jamhuri ya Kenya. Sasa watu wanaangalia ile bendera ya Kenya Raila alikuwa nayo pale ni the same bendera watoto walikuwa wanabeba na chupa ya maji na kufanya valid demonstrations na kuwawawa, and no valid explanation. Kwa hivyo wakasema ni yule rais aliua watoto ndiye amewakilisha mgombeaji hapa,” Kalonzo alisema.
Zaidi ya hayo, alidai kwamba nguvu ya ushawishi ya Gen Z ilienea nje ya mipaka ya Kenya, na kuathiri mtazamo wa jumuiya ya kimataifa kuhusu serikali ya Ruto.
Kalonzo alipendekeza kuwa ripoti za ukatili wa polisi na utekaji nyara wa waandamanaji vijana ziliibua wasiwasi wa kimataifa, na kusababisha serikali za kigeni kuhoji kujitolea kwa Kenya kwa haki za binadamu.
Alidai kuwa, jambo hili lilizidisha ugumu wa kuwania kwa Raila, kwani mataifa ya kigeni yaliona kampeni yake kama nyongeza ya serikali ambayo ilihusishwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
"Wagombea hawa wachanga wana uwezo wa kushawishi mtu yeyote mahali popote, na walimshawishi mkuu wa nchi. Kwa hivyo nchi hizo zingine zikasema, ‘Nchi ambayo inaua watoto, nchi ambayo ni abductions.’ Kwanza hiyo ni mbaya sana. Hata heri ile kizuizini bila kufunguliwa mashtaka kwa sababu karatasi zako zilikuwa zikitiwa sahihi ambazo zimewekwa ndani,” Kalonzo alisema.
Kura za Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ambazo zilishuhudia Raila Odinga akishindwa na Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti zilifanyika Februari 15, 2025, baada ya mchakato wa uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Kinyang'anyiro hicho ambacho kilidumu kwa duru nyingi za upigaji kura, kilishawishiwa vikali, huku wagombea wakihangaika kupata kura 33 zinazohitajika kwa ushindi.
Licha ya uongozi wa mapema, uungwaji mkono wa Odinga ulipungua huku kinyang'anyiro hicho kikiendelea, na hivyo kumalizika kwa kujiondoa baada ya duru ya sita kwa kura 22, huku Mahmoud akishikilia 26.
Huku Raila akijipigia debe, Mahmoud aliingia kwenye kura ya mwisho, na hatimaye kunyakua uenyekiti wa AUC.