
KINARA wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka ameendeleza harakati zake za kumshambulia spika wa Bunge la kitaifa kwa kile anadai kwamba anahujumu haki ya Kidemokrasia ya kutotambua muungano wa Azimio kama wa walio wengi bungeni.
Akizungumza mapema Jumatano, Musyoka alisema kwamba spika
Moses Wetang’ula ni rafiki yake lakini wanaenda kumchukulia hatua za kisheria
kwa kutoheshimu uamuzi wa mahakama.
Spika huyo anatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu ni nani wanafaa
kuketi upande wa walio wengi na wachache katika bunge la kitaifa baada ya
mkanganyiko kushuhudiwa bungeni Jumanne katika kikao cha kwanza mwaka huu.
Musyoka pia alisema kwamba mapambano dhidi ya utawala wa rais
Ruto yataendelea huku akimtaka Raila Odinga iwapo atafeli kupata wadhifa wa AUC
arudishe nguvu zake katika harakati za kuikosoa serikali humu nchini.
“Hiyo vita inaendelea kwa
bunge itaendelea. Ule wizi waliibia Raila mahakama imeonyesha wazi kwamba
wabunge wengi ni wa Azimio. Spika anajaribu kujitetea na mahakama imesema
huwezi. Huyu spika ni rafiki yangu lakini anaenda kuitwa kwa kudharau mahakama,” Musyoka alisema.
“Raila anaenda kutafuta
kiti AU, namwambia aende lakini akiona kimeumana arudi hapa tukomboe nchi ya
Kenya,” Kalonzo aliongeza.
Siasa za ni mrengo upi ulio na uwakilishi mwingi bungeni
zimeshamiri nchini tangu mwishoni mwa wiki jana mahakama ilipoamua kesi iliyowasilishwa
kuhusu suala hilo.
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, muungano wa Azimio la Umoja
One Kenya ulikuwa na wawakilishi wengi kwenye mabunge yote mawili.
Hata hivyo, Septemba 2022 spika wa bunge Moses Wetang’ula
aliamuru kwamba UDA kilikuwa na uwakilishi mwingi na hivyo kukabidhiwa nyadhifa
za walio wengi bungeni.