
Viongozi wamtakia kila la heri Raila katika kiti cha AUC
Baada ya siku moja kutamatika kwa hafla iliyoandaliwa Jumatatu
Februari 10,2025 kwa ajili ya kumwombea Raila Odinga katika safari yake ya
kuchaguliwa kama mwenyekiti wa AUC.
Viongozi mbali mbali walijitokeza kumhongera na kumtakia kila
la heri katika uchaguzi huo ambao umeratibiwa kufanyika siku ya Jumamosi Februari 15,2025.
Wakili Nelson Havi alidokeza kuwa kulingana na historia pana
na uzalendo ambao bwana Odinga amekuwa nao kwa taifa letu la Kenya ikiwa Pamoja
na tajiriba ya uongozi alimsawiri Odinga kama chaguo bora la Kenya na la Afrika
kwa Jumla.
Seneta wa Nyandarua John Methu naye kwa upande mwingine alimtakia
kiongozi wa ODM kila la heri katika uchaguzi huo ujao ila alipinga pendekezo la
wabunge zaidi ya mia moja (100) ambao waliratibiwa kuandamana naye katika
safari ya Addisababa kule Uhabeshi.
Kulingana na kauli za bwana Methu aliwazia kuwa wabunge
zaidi ya 100 watakaofika Addisababa kwa hafla ya kushuhudia upigaji kura huo
ukifanyika alionelea kuwa hiyo ilikuwa ni kutumia ushuru wa wananchi vibaya na badala
yake alipendekeza akisema kuwa bwana Odinga ana usimamizi wa uhazili wake ambao unastahili kuwa umetenga bajeti kwa
ushirikiano na kamati andalizi ya masula ya kigeni ili kufanikisha kila kitu
bila kugusa pesa za mlipa ushuru.
Kwa upande mwingine naibu Sipika katika bunge la taifa bi
Gladys Boss Shollei alimmiminia sifa bwana Odinga akimtaja kama mzalendo na mtu
mwenye utu zaidi wa kupenda nchi yake kuliko maslahi yake alisema hayo
akihojiwa na kituo kimoja cha runinga humu nchini.
Bi Sholei alikariri kuwa kulingana na historia ya Raila
Odinga ya siasa yeye ndiye mtu ambaye anayafahamu masuala ambayo huwaathiri
wananchi sana na pia anatajiriba pana katika uongozi.Alikuwa akieleza jinsi Raila
alivyokuwa mhimili imara katika serikali za mwanzoni alitaja serikali ya Moi,Kibaki,Uhuru
na Ruto.
Hata hivyo katika hotuba ya bwana Odinga siku ya Jumatatu
kwa hafla ya maombi ya kumwombea, Odinga alisema yuko tayari kuongoza bara la
afrika akikariri kuwa ana matumaini ya kuibuka na ushindi.