

PETER Kaluma, mbunge wa Homa Bay Mjini ameendelea kutetea msimamo wake kuhusu suala la kupashwa tohara kwa watoto wa kiume.
Kwa siku mbili mfululizo sasa, mbunge huyo amekuwa akipigia
debe desturi ya kupasha tohara wanaume kupigwa marufuku nchini Kenya.
Baada ya kuweka chapisho la kutaka tohara ya wanaume kupigwa
marufuku akisema kwamba inafuata itikadi za kizamani kwenye Biblia wakati wa
Abrahamu, Kaluma amerudi akisema kwamba tohara ya wanaume hufanywa na takribani
asilimi 10 tu.
“Ulimwenguni kote, tohara
inafanywa na takriban 10% ya wanaume wadogo, dhaifu na wachafu. Tukomeshe aina
zote za ukeketaji nchini Kenya na kuwaepusha vijana wetu na maovu haya ya
kijamii,” alitoa wito.
Ameibua madai mengine akisema kwamba visa vya wasichana
kupata mimba za mapema vimejaa katika jamii ambazo zinafanya tohara kwa
wanaume.
Alitoa changamoto kwa jamii hizo akihoji kwa nini wanapasha
tohara watoto wao wa kike kisha kukimbia kuwatafuta wanawake kutoka jamii za
wasiokeketwa kama kweli wanaamini tohara ni jambo la maana.
“Ukeketaji, mimba za utotoni na ndoa za utotoni zimeongezeka katika jamii nyingi zinazofanya ukeketaji (tohara). Kwa nini wanaume kutoka katika jamii zinazofanya ukeketaji wakakata sehemu za siri za mabinti zao kisha kuwakusanya wanawake kutoka katika jamii ambazo hazifanyi hivyo, kama ukeketaji ni mzuri!” Kaluma aliongeza.
Awali, Kaluma alikuwa ametaka kutupiliwa mbali kwa desturi ya
kupasha tohara wanaume, akisema kwamba katika jamii zote za wanyama, binadamu
tu ndio wanatahiri, jambo ambalo aliliona si sawa.
‘Acha kutahiriwa. Tohara
ni kukata wanaume. Punda hawatahiri. Wanyama wote hutahiriwa isipokuwa wanadamu
wachache ambao wamedanganywa kwamba wao ni wajukuu wa Abrahamu, mtu aliyeishi
jangwani bila maji!” alisema.
Hata hivyo, maoni yake yamepokea pingamizi kali kutoka kwa
watumizi wa mitandao ya kijamii, wengi wakidai kwamba tohara humfanya mtu kuwa
msafi kinyume na Kauli yake kwamba wanaume wachache wanaotahiri ni wachafu na
wadhaifu.