

MAMLAKA ya kitaifa ya usafiri na usalama barabarani NTSA imetangaza kupiga marufuku kampuni ya magari ya Super Metro ambayo hufanya biashara ya uchukuzi wa umma jijini Nairobi na kaunti majirani.
Kupitia tangazo lililochapishwa kupitia ukurasa wao wa X,
NTSA ilitaarifa umma kwamba sacco hiyo yenye magari ya uchukuzi wa umma zaidi
ya 500 yamepigwa marufuku kutoka barabarani hadi pale watakapozingatia
kikamilifu Kanuni za Magari ya Utumishi wa Umma ya 2014 na masharti mengine
yaliyowekwa.
“Hii ni kuufahamisha Umma
kwamba Mamlaka imesimamisha leseni ya waendeshaji wa Super Metro Limited hadi
Kampuni itii kikamilifu Kanuni za Magari ya Utumishi wa Umma, 2014 na masharti
mengine yaliyowekwa,” sehemu ya chapisho hilo ilisema.
NTSA ilionya watumizi wa usafiri wa umma dhidi ya kuabiri gari
lolote la sacco hiyo huku agizo likitolewa kwa maafisa wa Trafiki kuyazuia
magari yao yote yatakayopatikana yakibeba abiria barabarani.
“Wananchi
wametahadharishwa dhidi ya kupanda gari la kampuni ya Super Metro Limited.
Idara ya Trafiki inahitajika kukamata magari ya Kampuni ambayo yatapatikana
yakifanya kazi kinyume na kusimamishwa,” tangazo hilo lilisomeka
zaidi.
Haya yanajiri siku chache kufuatia tukio la kuhuzinisha
ambapo mwanamume wa umri wa makamo aliripotiwa kufa baada ya kudaiwa kusukumwa
kutoka ndani ya moja ya gari la sacco ya Super Metro likiwa katika mwendo wa
kasi.
Kulingana na NTSA ilifanya uchunguzi wa kina kwenye Super Metro
na kubaini kuwa kati ya magari yake 523, 15 yalikuwa na vyeti vya ukaguzi vilivyokwisha
muda wake na 8 kati yao yalikuwa na Leseni za Huduma za Barabarani (RSL)
zilizoisha muda wa matumizi.
NTSA pia iligundua kuwa madereva kadhaa kutoka SACCO hawafikii
vigezo vinavyohitajika jambo ambalo linaleta hatari kubwa ya usalama.
Kabla ya leseni ya uendeshaji kurejeshwa Super Metro imeombwa
kuwasilisha magari 294 yenye ukiukaji kwa ukaguzi wa utiifu katika kituo cha
Ukaguzi wa Magari cha Likoni na kupata ripoti za kufuata sheria za magari yote.
Ni lazima pia iwasilishe madereva 42 kati ya 109 walio na
ukiukaji wa kasi ili wajaribiwe tena katika Kituo cha Majaribio ya Madereva
Likoni.
Hii ni baada ya madereva 64 kutoka Super Metro kushindwa kufanya majaribio tena mnamo Machi 10, na kusababisha kusitishwa kwa leseni zao za udereva.