
Kampuni ya kusimamia mabasi ya Super Metro imejitokeza na kutoa tamko rasmi kufuatia kifo cha abiria mmoja aliyeripotiwa kutupwa kutoka kwa basi lao lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo kasi katika eneo la Kahawa Wendani.
Katika taarifa yao ya Jumatano, Machi 12, kampuni hiyo ilieleza masikitiko yao makubwa kuhusu tukio hilo, ikituma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, Gilbert Thuo Kimani.
"Tunasikitishwa na tukio hili la kusikitisha. Mawazo yetu yako kwa familia na wapendwa wa mwathiriwa katika kipindi hiki kigumu," ilisoma sehemu ya taarifa hiyo.
Super Metro ilisisitiza kuwa inachukulia usalama wa abiria kwa uzito mkubwa na haikubaliani na vitendo vya uzembe au ukatili kutoka kwa wahudumu wao.
Kampuni hiyo ilitangaza kuwa wahusika wa tukio hilo wamesimamishwa kazi mara moja huku uchunguzi ukiendelea.
"Tunaelewa kuwa umma umeghadhabishwa, na kwa haki kabisa. Hakuna mtu anayepaswa kupoteza maisha kwa njia ya kikatili namna hii. Tunashirikiana kikamilifu na mamlaka ili kuhakikisha haki inatendeka," taarifa hiyo iliongeza.
Super Metro pia ilisema kuwa imechukua hatua madhubuti za kuimarisha mafunzo kwa wahudumu wake ili kuzuia matukio kama haya kutokea tena.
Ingawa uchunguzi rasmi bado unaendelea, ripoti za awali zilizosambaa mitandaoni zinadai kuwa Gilbert alifariki baada ya makanga wa basi hilo kumtupa nje kwa madai ya kuwa na nauli pungufu.
Kwa mujibu wa simulizi zilizotolewa na kusambazwa mitandaoni, abiria huyo alihitajika kulipa KSh 80 kama nauli, lakini alikuwa na KSh 50 pekee. Mabishano kati yake na makanga yalizidi, na ndipo kisa hicho cha kusikitisha kinadaiwa kutokea.
Ripoti hizo zinaeleza kuwa basi lilipokuwa likipita eneo la Kahawa Wendani kwa mwendo kasi, makanga huyo alifungua mlango ghafla na kumtupa abiria huyo nje.
Pia inadaiwa kuwa matokeo ya upasuaji wa mwili yanaonyesha marehemu alivunjika mbavu zote, mikono na miguu, jambo lililosababisha kifo chake papo hapo.
Tukio hilo limezua hasira kali miongoni mwa wanamitandao na wananchi kwa jumla, huku wengi wakitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya mhusika.
Kwa sasa, familia ya marehemu inasubiri uchunguzi rasmi wa
mamlaka ili kuhakikisha haki inatendeka kwa mpendwa wao.