
MJASIRIAMALI Anerlisa Muigai ni Mtu maarufu wa hivi punde kutoa tamko lake kuhusu wale wanaodhihaki na kukejeli kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, Wafula Chebukati.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram wikendi iliyopita, Muigai
aliwataka wale wanaodhihaki kifo cha Chebukati kuwa na utu, akisema kwamba kifo
kinaweza mpata mtu yeyote yule wakati wowote bila kujali majira na wakati.
Muigai aliwataka watu kuwa na utu kwa kuifariji familia ya
Chebukati badala ya kukejeli kifo chake, kwani kwa kufanya hivyo wanaongezea
msumari moto kwenye kidonda.
“Nyinyi wote ni kama mmesahau kwamba alikuwa baba, mume, babu, rafiki, mjomba, kiongozi, n.k. Kwa nini mtu yeyote amcheke/kumdhihaki? Kifo ni cha kibinafsi/nyeti sana. Watu wanapaswa kuwa na heshima, haswa kwa sababu kuna familia zinazoomboleza,” aliandika.

Kauli ya Muigai ilijiri siku moja tu baada ya afisa mkuu
mtendaji wa MCSK, Ezekiel Mutua kuwakosoa wakenya ambao walifurika kwenye
mitandao ya kijamii kudhihaki kifo cha Chebukati aliyefariki mwishoni mwa wiki
jana.
Mutua alishangazwa ni kwa nini kizazi cha sasa kimefikia
hatua ya kupanda mbegu za hasira na kisasi mioyoni mwao kiasi kwamba wanamtakia
kifo mpaka mtu ambaye tayari ni marehemu.
“Tulifilisikaje kimaadili hadi tukawasema vibaya wafu, tukawachukia
watu hadi kuwatakia kifo hata wakiwa wamekufa? Tumepoteza ubinadamu wetu?
Tutaipataje tena kama nchi?" Mutua aliweka pozi.
Chebukati alifariki akiwa anapokea matibabu katika hospitali
moja jijini Nairobi akiwa na umri wa miaka 63 na familia yake iliomba faragha
wanapomuomboleza mpendwa wao.
Katika video ya kutia huruma iliyoonekana na meza yetu ya
habari, mwanawe Chebukati, Emmanuel Chebukati aliwaomba Wakenya kuacha
kudhihaki kifo cha baba yake, akiwataka wamsamehe kama aliwakosea.
"Sijawahi kuona Wakenya wakiungana
kusherehekea kifo cha Mkenya mwenzangu kwani nimeona watu wakifurahi na
kutudhihaki," alisema.
"Kwa mara ya
kwanza, nimeona Wakenya wakisherehekea kifo cha mtu fulani-sio kifo cha mtu wa
kawaida, lakini kile cha kiongozi ambaye alichukua jukumu muhimu katika
kuendeleza demokrasia ya nchi."
Alifanya kazi yake kwa heshima na kwa
kuzingatia katiba kwa sababu baba yetu alithamini sheria na hakuwahi kwenda
kinyume," kijana huyo
aliongeza.
“Hakuwahi kufanya maamuzi
kutokana na hisia zake binafsi bali alifuata sheria na katiba kila mara. Labda
mambo hayakwenda kama baadhi ya Wakenya walivyotarajia, na kwa sababu
alishikilia sheria, sasa wanatudhihaki mtandaoni.”