
WAZIRI wa masuala ya usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen amemuomboleza aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, Wafula Chebukati kama mtu mkakamavu.
Murkomen alizungumza na vyombo vya habari saa chache baada ya
taarifa kufichuka kwamba Chebukati amefariki.
Alimsifu Chebukati kama mtu ambayo aliacha alama ya kipekee
katika kipindi chake cha miaka 6 kwenye tume hiyo.
“Wafula Chebukati
atakumbukwa kwa uongozi wake wenye kanuni kanuni, ujasiri na uaminifu kwa
Katiba. Akiwa mzalendo wa kweli na mtu mwadilifu sana, Chebukati aliongoza Tume
Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kupitia chaguzi mbili kitaaluma,” Murkomen aliandika
kwenye X.
Pia alitoa wito kwa kamati itakayoongoza mchakato wa
kuwachagua makamishna na mwenyekiti wa IEBC kuhakikisha kwamba tume hiyo inapata
mwenyekiti mwenye misimamo ya kweli kama Chebukati.
Kwa mujibu wa Murkomen, Chebukati alisimama kidete kutetea
ukweli wa kikatiba bila kuyumbishwa, akisema kwamba hata IEBC ya sasa inafaa
ipate mwenyekiti kama yeye.
“Naomba kwamba ile kamati
ambayo inatafuta mwenyekiti wa IEBC ihakikishe kwamba imetafuta vile vigezo
ambavyo vilikuwa kwa Chebukati. Kwa sababu tunataka mtu ambaye hawezi
akatishwa.”
“Mtu ambaye hawezi tishwa
na upande wa serikali na hawezi tishwa na upande wa upinzani kwa sababu yeye ni
refa lazima asimamie upanjde wa katiba, na ukisimama upande wa katiba huwezi
kosea,” Murkomen aliongeza.
Alisema kwamba IEBC inastahili mtu ambaye anasimamia ukweli
na kusikiliza ushauri wa kweli bila kutegemea maoni yake binafsi kufanya
maamuzi.
“Asikuwe ni mtu ambaye anafuata maoni yake binafsi, mtu ambaye hana uzalendo, mtu ambaye hazingatii mambo ya taifa, unajua kwamba sisi wenye tunasimamia mambo ya usalama, tishio kubwa ni wale ambao wanatenda mambo ya kuwakera wananchi. Kwa hivyo tunataka mtu mwenye atachaguliwa awe ni mwenye atasimamia katiba,” Murkomen alisema.
Chebukati alitangazwa kufariki mapema Ijumaa ya Februari 21
baada ya kuugua kwa muda katika hospitali moja jijini Nairobi.
Alifariki akiwa na umri wa miaka 64 na alihudumu kama
mwenyekiti wa IEBC kwa miaka 6, Januari 2017 hadi Januari 2023.