Rais William Ruto ametuma rambi rambi kwa ndugu jamaa na marafiki wa aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka Wafula Chebukati.
Ruto alimtaja Chebukati kama kiongozi aliyekuwa mwenye bidii na ambaye alitumikia taifa kwa uadilifu.
“Nimepokea habari za kuaga kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati kwa masikitiko makubwa. Chebukati alikuwa kiongozi mwenye kanuni na bidii aliyetumikia taifa kwa uadilifu. Kifo chake ni hasara kubwa kwa nchi yetu. Mawazo na sala zetu ziko pamoja na familia yake na marafiki katika kipindi hiki kigumu. Pumzika Kwa Amani,” rais aliandika kwenye mtandao wa X.
Chebukati alifariki saa tano usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa.
Alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali hiyo. Kile Chebukati alikuwa anaugua bado kinabaki kuwa cha faragha.
Chebukati alihudumu kama mwenyekiti wa IEBC kwa muhula mzima wa miaka sita na alistaafu Januari 2023.
Aliongoza Uchaguzi Mkuu wa 2017 na 2022.
Wakati wa uongozi wake, aliweza kusimamia chaguzi tatu za Kenya: uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2017, uchaguzi wa marudio wa urais wa Oktoba 2017 na uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2022.
Alikuwa wakili wa uzoefu wa miaka 37 na aliendesha kampuni yake ya uanasheria kwa zaidi ya miaka 20.
Mnamo 2006, Chebukati alianzisha kampuni ya uwakili Cootow & Associate Advocates, ambayo alijiuzulu mnamo Januari 17, 2017, kabla ya kuwa mwenyekiti wa IEBC.
Alitekeleza sheria za ushirika, sheria za kibiashara, utawala wa shirika na utatuzi wa migogoro.
Alikuwa mwanasiasa na mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), ambacho pia alijiuzulu, kabla ya kuomba nafasi ya mwenyekiti wa IEBC.