
MBUNGE wa Gatundu Kusini, Gabriel Kagombe ametoa wito kwa serikali kumpa aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC, Wafula Chebukati mazishi ya kitaifa kama shujaa.
Akizungumza Jumamosi, Kagombe alisema kwamba
Chebukati alisimama tisti kwa ujasiri kuhakikisha kwamba taifa la Kenya
halikutumbukia katika machafuko ya baada ya uchaguzi wa Agosti 2022, hivyo
anastahili heshima zote za kishujaa katika mazishi yake.
“Tutamkumbuka Chebukati kwa kuwa mtu
mkakamavu, mtu shupavu, mtu ambaye alipigania haki ya Wakenya, mtu ambaye
hakuogopa hata alipopewa vitisho vya woga alisimama kidete na kusema kwamba
haki ya Wakenya lazima ipatikane,” Kagombe
alitoa risala zake za rambirambi kwa marehemu Chebukati.
“Mimi nataka kumkumbuka kwamba mwaka
2022 tulikuwa katika hali mbaya ambapo nchi hii ingepasuka, vita vingetokea. Na
tunaona ya kwamba yeye alisimama kidete na kusema ukweli, yale ambayo yalileta
vita 2007 ni kwa sababu yule aliyekuwepo hakusimama kidete, lakini Chebukati
alisimama na kusema ukweli.”
“Mimi nasema kwamba Chebukati ni
shujaa ambaye anastahili kupatiwa heshima yake na mimi najua hata nchi hii na
serikali itampa mazishi ama buriani ya kufaa,”
Kagombe alijieleza.
Wafula Chebukati aliteuliwa kuwa mwenyekiti
wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta
Januari 2017.
Alisimamia uchaguzi mkuu wa 2017 na 2022,
ambapo alikabiliwa na changamoto kadhaa kabla ya kustaafu 2023.
Matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017
yalibatilishwa na Mahakama ya Juu kwa sababu ya kasoro zilizobainishwa, na
hivyo kuwa mara ya kwanza kwa uchaguzi wa urais kubatilishwa nchini Kenya. Hata
hivyo, Chebukati aliongoza tume hiyo kupitia uchaguzi wa marudio uliofuata.
Katika uchaguzi wa 2022, Chebukati
alimtangaza William Ruto kuwa Rais mteule licha ya migawanyiko ndani ya tume
hiyo ambayo ilizua taharuki kwa umma.
Alisimama kidete na matokeo yaliyotangazwa,
ambayo hatimaye yaliidhinishwa na Mahakama ya Juu.
Alipostaafu mnamo Januari 2023, Chebukati
alituzwa Mzee wa Agizo la Moyo wa Dhahabu (EGH), heshima ya pili ya juu ya
kiraia nchini Kenya, kwa kutambua utumishi wake.