
Mwanamuziki maarufu wa Mugithi, Samuel Muchoki almaarufu
Samidoh, ameomboleza kwa hisia kali kifo cha rubani mstaafu, Kanali (Mstaafu)
James Gitahi, aliyefariki katika ajali mbaya ya barabarani mnamo Alhamisi,
Machi 6.
Gitahi, ambaye alikuwa rubani wa ndege za kibiashara, alipoteza maisha baada ya gari lake kugongana na lori na kulipuka katika Barabara Kuu ya Mombasa.
Kupitia mitandao ya kijamii, Samidoh alieleza huzuni yake, akisema kifo cha Gitahi ni habari mbaya zaidi alizopokea. Alimtaja marehemu kama baba kwake na kueleza jinsi alivyomchukua kama mwanawe, kumtunza, na kushiriki naye mazungumzo yenye hekima.
"Leo imekuwa siku ngumu sana, kupokea habari mbaya zaidi. Mtu aliyenichukua kama mwanawe, kunijali, na kushiriki nami mazungumzo bora na mtazamo wa dunia, hayupo tena," aliandika Samidoh kwenye Instagram.
Mwanamuziki huyo wa nyimbo za Kikuyu alisema bado haamini kuwa Kanali Mstaafu Gitahi amefariki na ataikosa sana hekima yake ya kifadhila.
"Baba, bado siamini. Nitaikosa sana hekima yako ya kifadhila na tabia yako ya upole. Pumzika salama, Kanali (Mstaafu) James Gitahi," aliongeza.
Kwa mujibu wa polisi, Kanali (Mstaafu) James Gitahi alikuwa peke yake ndani ya gari aina ya saloon wakati ajali ilipotokea kwenye Barabara ya Mombasa.
Aliaga dunia papo hapo baada ya mwili wake kuteketea vibaya kwenye ajali hiyo iliyotokea saa kumi na moja unusu jioni.
Ingawa Gitahi alikuwa mstaafu wa urubani wa kijeshi, bado alikuwa akiendesha ndege za kibiashara katika Uwanja wa Ndege wa Wilson.
Mashuhuda walisema marehemu alikuwa safarini kuelekea Nairobi na alikuwa akijaribu kulipita lori alipogongana na lori lingine lililokuwa likija kwa mwendo wa kasi.
Kutokana na mgongano huo, gari lake lililipuka na kumfanya asalie ndani bila njia ya kujiokoa.
Juhudi za waokoaji hazikufua dafu, na familia yake ilipokea taarifa za kifo chake baada ya namba ya usajili ya gari lake kusambazwa. Mwili wake ulioteketea ulihamishiwa katika hifadhi ya maiti ya Machakos kwa uchunguzi zaidi.
Dereva wa lori lililogongana na gari la Gitahi alipata jeraha la kuvunjika mguu wa kushoto na alikimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Familia ya marehemu ilikuwa imepanga kuuhamishia mwili wake katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee Alhamisi.
Polisi wamesema wanaendelea na uchunguzi kuhusu ajali hiyo.