
KATIBU mkuu wa muungano wa wafanyikazi nchini COTU, Francis
Atwoli amefananisha cheo chake kama cheo cha kuhani wa kanisa Katoliki.
Atwoli aliibua mfanano huo kupitia ukurasa wake wa X
alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa aliyekuwa gavana wa Makueni, profesa
Kivutha Kibwana.
Akielezea safari yake katika kupigania haki za wafanyikazi hadi kufikia kuteuliwa kama katibu wao mkuu, Atwoli alisema kuwa kuwa katibu ni safari ya kukwea ngazi kama vile padre wa Katoliki anayekwea ngazi haki kufikia cheo cha Upapa.
“Kabla sijawa kiongozi wa
chama cha wafanyakazi nilifanya kazi katika shirika la bango na mawasiliano la
Kenya ambapo nilihudumu kwa miaka 19 na kisha miaka 7 kama Mkurugenzi wa
Shirika katika COTU (K),” Atwoli alisema.
“Kuhudumu kama Katibu
Mkuu wa COTU (K) ni wito. Ni sawa na Padre wa Kikatoliki kupanda vyeo na kuwa
Papa katika Vatican. Masharti na mwenendo wetu wa utumishi umeegemezwa kwenye
wito wa Mungu,” aliongeza.
Akionekana kudokeza kuwa bado hajachoka na uongozi wa
muungano wa wafanyikazi, Atwoli alisema kwamba maadam wafanyikazi wana furaha
chini ya uongozi wake, haoni haja ya kung’atuka.
“Na ili mradi bado nina
uwezo na wenzangu bado wanafurahia utumishi wangu wataendelea kunichagua hadi wakati
huo wafikirie vinginevyo,” alikariri msimamo.
Awali, alifichua kuwa chini ya uongozi wake, wafanyikazi wa
kiume nchini sasa wanapata likizo za uzazi, kinyume na ilivyokuwa awali kabla
ya ujio wa katiba ya 2010.
“Kwanza, nimepigania wafanyikazi [wa kiume] wa Kenya
kupokea likizo ya uzazi kama sehemu ya kazi yangu kuleta seti tano (5) za
sheria za Kazi. Unatambua kwamba sheria hizi na Katiba ya Kenya 2010, kama
ilivyo katika Kifungu cha 41, zimempa mfanyakazi Mkenya mamlaka zaidi ya yote
katika eneo hili,” alisema.
Mapema wiki jana, Francis Atwoli,75, aliripotiwa kukaribisha
mtoto na mkewe Mary Kilobi, 40, baada ya kuwa katika ndoa kwa takribani miaka 7.