
WAZIRI wa Ulinzi, Roselinda Soipan Tuya ametuma maafisa wa jeshi, KDF katika kaunti ya Mombasa kuongeza nguvu katika shughuli za ubomozi wa jumba la ghorofa 11 lililoanza kuzama mapema mwezi huu.
Waziri Tuya alichapisha rasmi notisi hiyo
katika gazeti la serikali mnamo Aprili 7 kuhusu kutumwa kwa KDF katika
kuendesha shughuli hiyo ambayo inatarajiwa kufanyika Aprili 9.
Jumba hilo la ghorofa 11 lililopo eneo la
Kilifi Corner lilianza kuzama mnamo Aprili 2 na kuweka maisha ya wakaazi na
majirani wake katika hali ya hatari.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 241 (3) (b)
cha Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, Pamoja na ibara ya 31 (1) (a), (c) na 34 (2)
ya jeshi la Kenya KDF, notisi inatolewa kwamba mnamo Aprili 7, 2025, KDF
walitumwa kusaidia wizara ya ndani na kaunti ya Mombasa katika hali ya dharura
ambapo jumba la ghorofa 11 lililopo Kilifi Corner katika Barabara ya Abdel
Nasser ambalo lilianza kuzama Aprili 2 hivyo kuweka hatarini maisha ya wakazi
wa majumba yaliyo karibu nalo,”
notisi hiyo katika gazeti la serikali ilisomeka.
Gavana wa Mombasa, Abdullswamad Sherrif
Nassir alithibitisha kuendeshwa kwa shughuli hiyo ya kuliangusha chini ghorofa
hilo ambalo limetajwa kuwa tayari orofa ya chini imezama kabisa.
Operesheni ya kubomoa jengo hilo ilianza
mapema Jumatano na inatarajiwa kuchukua karibu saa 8, kwani wakaazi wanaoishi
karibu wametakiwa kuondoka katika nyumba zao katika eneo hilo ili kuruhusu
operesheni salama.
Kulingana na Gavana wa Mombasa Abdullswamad
Sheriff Nassir, wagonjwa mahututi katika hospitali ya Makadara watahamishwa kwa
muda katika vituo vya afya vilivyo karibu kabla ya ubomozi kuanza.
"Watu hawafai kwenda kazini
kilomita 1.2 karibu na jengo," Gavana
alibainisha akitaja maeneo kama soko la Marikiti, Buxton na City Blue.
"Watu wote walio karibu watalazimika
kuondoka. Hii haitaathiri nyumba yako lakini mitetemeko itaathiri masikio yako
ikiwa uko karibu. Wale ambao watafanya kazi hiyo watakuwa na vifaa vya
kujikinga."