
Rais William Ruto amepuuza kwa ujasiri vitisho kutoka kwa upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, akiahidi kushughulika na wapinzani wake wa kisiasa “asubuhi na mapema.”
Akizungumza Jumamosi, Rais alionya kuwa hakuna kiwango cha vitisho au propaganda kitakachozuia ajenda ya maendeleo ya serikali yake.
“Nimekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu. Na hakuna mtu anayeweza kunitisha. Ati kutishwa? Hapana, watafute mtu mwingine,” Ruto alisema, akipuuza mikutano ya upinzani ya hivi karibuni na wito wa kujiuzulu kwake.
Alikuwa akizungumza katika Maonyesho ya Kumi ya Wakulima wa Maziwa ya Mwaka 2025, katika uwanja wa maonyesho wa ASK Meru.
Ruto aliwashambulia wakosoaji wake wa kisiasa, akiwashutumu kwa kukosa mpango wa maendeleo kwa Wakenya.
“Wanachojua ni ‘Ruto must go’. Porojo, propaganda tu... ooh Kasongo, sijui Ruto must go. Hawa watu hawana mpango wowote kwa Wakenya,” alisema Rais.
Kiongozi wa taifa alisisitiza kuwa serikali yake imejikita katika kuunganisha taifa na kutekeleza ahadi zake.
Alisisitiza kuwa wale wanaotaka kuanza kampeni za 2027 wanaweza kuendelea, lakini yeye ataendelea kushughulikia utoaji huduma kwa wananchi.
“Hii serikali itaendelea kuendeleza nchi, na ndio maana nimesema nitamkaribisha yeyote ambaye yuko tayari kufanyia Wakenya kazi,” alisema.
“Lakini kwa wale wanaotaka kufanya kampeni, waendelee. Si 2027 tutakutana nao? Kwani ni mafundi kiasi gani?”
Ruto pia alimsifu naibu wake, Kithure Kindiki, kwa kuwa na mtazamo na kuelewa wajibu wake, akimtofautisha na viongozi wa zamani aliowataja kuwa walikuwa watu wa maneno mengi bila vitendo.
“Kwa sasa angalau nina naibu ambaye anajua na kuelewa majukumu yake. Sio mtu wa kuzungumza tu kila wakati,” alisema.
Akiwaalika Wakenya kushikamana, Ruto alitoa wito kwa wananchi kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya serikali yake.
“Tunajua umoja ni nguvu, kujitenga ni udhaifu. Ndio sababu mimi kama kiongozi wa taifa hili, nitawaunganisha Wakenya wote, tuweze kutembea safari moja,” alieleza.
Kauli za Rais Ruto zinajiri wakati ambapo shughuli za kisiasa kutoka kwa upinzani zimeongezeka.
Ruto alisema kwamba hatishwi, akisisitiza kuwa serikali yake imejikita katika utendaji kazi na ushirikishwaji, na iko tayari kukumbana na debe wakati utakapowadia.
Matamshi haya yanakuja muda mfupi baada ya Ruto kusema wazi kuwa hatawahi kukabidhi mamlaka kwa upinzani katika mwaka wa 2027.
Akizungumza Juni 15, huko Kakamega, alisema hawezi kukabidhi madaraka kwa upinzani akidai hauna mpango wowote wa kuendeleza taifa.
“Hawa watu wengine (upinzani) hawana mpango, msipoteze muda kwao. Hatutakabidhi mamlaka kwa watu wasio na mpango. Mpango wao pekee ni kusema ‘Ruto must go’,” alisema Ruto.