
Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, amezitaka mamlaka kuwawajibisha waandalizi wa maandamano ya kizazi cha Gen Z yaliyopangwa kufanyika Jumatano, Juni 25, 2025, iwapo kutatokea upotevu wa maisha.
Kupitia chapisho kwenye mtandao wa X mnamo Jumatatu, Juni 23, 2025, seneta huyo mashuhuri alitoa kauli hiyo wakati ambapo vijana wengi wamekuwa wakitoa wito wa maandamano ya kitaifa kulaani ukatili wa polisi na mauaji ya kiholela.
Alibainisha kuwa ingawa Ibara ya 37 ya Katiba inaruhusu maandamano ya amani na bila silaha, pia inalinda raia dhidi ya madhara.
“Waandalizi na wafadhili wa maandamano ya kizazi cha Gen Z lazima wawajibishwe kibinafsi endapo maisha yatapotea, mali kuharibiwa au amani kuvurugwa nchini,” alisema Cherargei.
Seneta huyo ambaye ni mshirika wa muungano tawala wa United Democratic Alliance (UDA), pia aliwaonya Wakenya dhidi ya kuandamana kuelekea Ikulu ya Nairobi — makazi rasmi na kitovu cha mamlaka ya Rais.
“Ikulu ni eneo lililolindwa kisheria na hairuhusiwi maandamano kufanyika humo,” alionya Cherargei.
Wakati uo huo, aliitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya mashirika ya kiraia yanayodaiwa kufadhili maandamano hayo.
“Bodi ya usimamizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali lazima yafute usajili wa mashirika ya wanaharakati yanayoeneza machafuko kupitia maandamano ya vurugu,” alisema.
Kauli ya Cherargei ilitolewa siku hiyo hiyo ambapo Msemaji wa Serikali, Isaac Mwaura, alipuuza ripoti za maandamano yaliyopangwa kufanyika Juni 25, akisisitiza kuwa siku hiyo itakuwa ya kawaida ya kazi.
Akizungumza Jumatatu, Juni 23, 2025, Mwaura alisema kwamba ingawa Wakenya wana uhuru wa kuadhimisha siku hiyo kwa njia ya binafsi, serikali haitaruhusu maandamano ya hadharani.
“Hakutakuwa na maandamano Juni 25. Siku hiyo itakuwa siku ya kazi kama kawaida,” alisema Mwaura.
“Mtu yeyote anayetaka kuadhimisha siku hiyo anaweza kufanya hivyo — akiwa nyumbani.”
Mwaura alilaani vikali kile alichokitaja kuwa “utekwaji wa kihalifu” wa maandamano hayo na watu wenye nia ovu wanaotumia maandamano hayo kama kisingizio cha kufanya vurugu na uharibifu.
Alisisitiza kuwa ni jukumu la polisi kuhakikisha usalama wa Wakenya wote na akawahimiza maafisa wa usalama kutekeleza majukumu yao kwa haki bila upendeleo wa kisiasa.
“Ni kosa kwa waandamanaji kubeba silaha, sawa na ilivyo kosa kuwadhalilisha au kuwachokoza polisi,” alisema.
“Iwapo mtu ataamua kuandamana, lazima afanye hivyo kwa amani na kwa kuzingatia sheria.”