
Baba wa Albert Ojwang, Meshack Opiyo, aliwasili katika Mahakama ya Kibera Jumanne kabla ya kuanza kwa kusikilizwa kwa kesi ya mauaji ya mwanawe.
Hii inajiri siku moja baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya maafisa wa polisi watatu wanaohusishwa na mauaji ya mwanablogu huyo.
Maafisa hao ni Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nairobi Central, OCS Samson Talaam, pamoja na makonstebo James Mukhwana na Peter Kimani, ambao watashtakiwa pamoja na raia wengine watatu.
Raia hao ni John Ngibe Gitau almaarufu Kinara, Gin Ammitou Abwao almaarufu Gilbeys, na Brian Mwaniki Njue, waliokuwa kizuizini katika kituo hicho cha polisi kabla ya kulipwa ili "kumfundisha adabu" marehemu, lakini waliishia kumuua katika harakati hizo.
"Taarifa kwa mshitakiwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa niaba ya Jamhuri ni kwamba washukiwa waliotajwa hapo juu wameshtakiwa kwa kosa lifuatalo – mauaji kinyume na kifungu cha 203 kikisomwa pamoja na kifungu cha 204 cha Kanuni ya Adhabu," sehemu ya hati ya mashtaka inasomeka.
"Usiku wa tarehe 7 Juni 2025, kati ya saa 3:30 usiku na saa 8:00 alfajiri katika Kituo cha Polisi cha Central ndani ya jiji la Nairobi, kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walimuua Albert Omondi Ojwang," sehemu ya mashtaka inasema.
Jaji Diana Mochache aliagiza washukiwa waendelee kuzuiliwa katika vituo walivyokuwa wakishikiliwa wakati wa uchunguzi.
Washukiwa hao wanadaiwa kumuua marehemu akiwa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nyumbani kwake Homa Bay.
Marehemu alikuwa amekamatwa na maafisa wa DCI kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat, kuhusu unyanyasaji wa kimtandao dhidi yake.