
Takriban watu wanane walipoteza maisha yao wakati wa maandamano yaliyofanyika kote nchini kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja wa maandamano ya kizazi cha Gen Z.
Kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR), vifo vyote vilisababishwa na majeraha ya risasi.
Tume hiyo ilisema kuwa vifo hivyo vilitokea katika kaunti sita: Machakos (2), Makueni (2), Nakuru (1), Kiambu (1), Uasin Gishu (1), na Nyandarua (1).
KNCHR ilieleza wasiwasi mkubwa kuhusu kile ilichokitaja kama “ukiukaji unaoendelea wa haki za binadamu na kutotii utawala wa sheria na taasisi za serikali pamoja na baadhi ya makundi ya raia.”
“Haki ya uhai ni takatifu. Tunatoa rambirambi kwa familia za waliofariki na tunazitaka pande zote kuheshimu umuhimu wa maisha,” alisema Naibu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dkt. Raymond Nyeris.
Mbali na vifo hivyo, tume iliripoti kuwa zaidi ya watu 400 walijeruhiwa, wakiwemo waandamanaji, maafisa wa polisi, na wanahabari.
Ingawa wengi wa waliojeruhiwa walipata matibabu na kuruhusiwa kuondoka hospitalini, watu 83 walihitaji matibabu ya kitaalamu, huku wanane wakiwa na majeraha ya risasi.
Maandamano hayo, ambayo yalifanyika katika angalau kaunti 23, yalishuhudia ulinzi mkali kutoka kwa vikosi vya polisi.
KNCHR ilibaini kuwepo kwa madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na vyombo vya usalama, ikiwemo kutumia risasi za mpira, risasi za moto, na magari ya maji ya kuwasha.
“Kuna ripoti za kuaminika kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi, ambayo yamesababisha majeraha mengi,” ilisomeka taarifa hiyo.
Tume pia ilielezea hofu juu ya kuingiliwa kwa maandamano hayo na wahalifu, hali iliyosababisha ghasia, uporaji, na uharibifu wa mali katika baadhi ya miji.
Zaidi ya hayo, KNCHR ililaani agizo lililotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano (CA) la kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano hayo, ikilitaja kama ukiukaji wa haki za kikatiba kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na upatikanaji wa habari.
“Tutaendelea kufuatilia hali na kutoa taarifa kwa wakati kuhusu uendelezaji na ulinzi wa haki za binadamu nchini katika kipindi hiki,” alihitimisha Dkt. Nyeris.