logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Junet Awasifia Wafuasi wa ODM kwa Kuepuka Ghasia Siku Ya Maandamano

Kupitia taarifa aliyoitoa siku ya Alhamisi, Junet alisisitiza umuhimu wa “maandamano ya amani".

image
na Tony Mballa

Habari26 June 2025 - 16:48

Muhtasari


  • Kauli yake ilijiri siku moja baada ya Gavana wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o, pia kuwapongeza wakazi wa kaunti hiyo kwa kuepuka maandamano hayo.
  • Katika taarifa iliyotolewa na afisi ya gavana, Nyong’o aliwasifu wakazi kwa kujiheshimu na kuendesha shughuli zao kwa utulivu.

Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, amewasifia wafuasi wa ODM kwa kujiepusha na maandamano ya Jumatano ambayo yalitawaliwa na machafuko, uharibifu wa mali na uporaji wa maduka jijini Nairobi na sehemu nyingine za nchi.

Kupitia taarifa aliyoitoa siku ya Alhamisi, Junet alisisitiza umuhimu wa “maandamano ya amani".

“Ninawapongeza wakazi wa Suna Mashariki na Migori kwa kudumisha amani wakati wa maandamano ya jana, hali iliyowaruhusu wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao kama kawaida,” alisema Junet.

“Katika ODM, tunakaribisha maandamano ya amani na tunawapongeza Wakenya kwa kutumia haki yao jana,” aliongeza.

Kauli yake ilijiri siku moja baada ya Gavana wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o, pia kuwapongeza wakazi wa kaunti hiyo kwa kuepuka maandamano hayo.

Katika taarifa iliyotolewa na afisi ya gavana, Nyong’o aliwasifu wakazi kwa kujiheshimu na kuendesha shughuli zao kwa utulivu.

Alibainisha kuwa mitaa ya Jiji la Kisumu na maeneo mengine ya kaunti hiyo ilisalia tulivu kwa kiasi kikubwa siku nzima.

“Ningependa kuwashukuru wakazi wa kaunti ya Kisumu kwa kudumisha amani leo wakati wa shughuli za kuadhimisha mwaka mmoja wa maandamano ya Gen Z,” alisema.

Gavana aliongeza, “Wakazi wa Kisumu daima watakuwa makini kulinda na kukuza haki za binadamu katika jamhuri yetu.”

Pia alisisitiza kujitolea kwa kaunti katika kushiriki mijadala ya kiraia yenye kujenga.

“Tutaendelea kueleza kutoridhika kwetu kwa njia ya kujenga dhidi ya aina yoyote ya ukandamizaji wa kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu.”

Maandamano ya Gen Z, yaliyolipuka katikati ya mwaka 2024, yaliendeshwa na vijana wa Kenya waliotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano ya kitaifa kupinga hatua mpya za ushuru na utawala mbaya.

Nyanza, ambayo mara nyingi huchukuliwa kuwa kitovu cha harakati za kisiasa, ilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyoshuhudia mvutano mkubwa wakati wa wimbi la kwanza la maandamano hayo.

Hata hivyo, mwaka huu, eneo hilo lilisalia na utulivu, huku wakazi wakiendelea na shughuli zao za kawaida japo maandamano ya kuadhimisha siku hiyo yalishuhudiwa katika kaunti nyingine.

  Baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu waliokuwa wakizungumza na wanahabari walivurugwa na vijana waliokuwa wakitumia pikipiki, ambao baadaye waliondoka.

Hakuna tukio kubwa lililoripotiwa eneo la Nyanza.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved