
Askari polisi Emily Kinya, aliyenusurika kifo kwa tundu la sindano baada ya kushambuliwa na waandamanaji wakati wa maandamano ya Jumatano iliyopita jijini Nairobi, ameeleza masaibu aliyopitia.
Kinya alikuwa miongoni mwa maafisa waliotumwa katika Barabara ya Muindi Mbingu kudhibiti umati uliokuwa ukiadhimisha kumbukumbu ya maandamano ya kupinga serikali yaliyofanyika mwaka jana.
Katika video iliyosambaa sana, anaonekana akikimbia pamoja na maafisa wengine wasio na silaha, kisha akajikwaa na kuanguka huku waandamanaji wakimkimbiza.
“Waandamanaji walituzidi nguvu,” alisema akiwa kitandani hospitalini anakoendelea kupokea matibabu.
“Wakati tulikuwa tunajiondoa, nilipigwa kwenye mguu, kisha nikaanguka. Ndipo waliponifikia.”
Kwa mujibu wa Kinya, aliyejiunga na Huduma ya Polisi ya Kitaifa mwaka 2013, baadhi ya waandamanaji walihamasisha wenzao wamuue alipokuwa amelala chini bila msaada.
“Kwa bahati nzuri, wachache walijaribu kunikinga. Lakini kulikuwa na wengine nyuma waliokuwa wakiendelea kunipiga na kuimba, ‘Tumuue. Wametuuwa mmoja wetu’.”
Kinya, mama wa watoto wawili, alipata jeraha la kichwa na majeraha kwenye tishu laini ya mguu wake.
Pia alipoteza simu yake ya mkononi na sare za polisi katika vurugu hizo.
Hatimaye aliokolewa na baadhi ya waandamanaji waliompeleka kwenye gari la wagonjwa lililokuwa limeegeshwa huku akivuja damu.
Hata hivyo, Kinya alikuwa na ujumbe kwa waandamanaji. Alisema watoto wake wamepata mshtuko mkubwa kutokana na yaliyotokea siku hiyo.
“Sisi pia ni binadamu. Maisha yetu ni ya thamani,” alisema.
Kwa mujibu wake, “Ilikuwa hali ya kusikitisha sana. Ilikuwa fupi lakini mbaya. Hata huwezi kuelewa kilichotokea hasa.”
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen tangu wakati huo amelaani shambulio hilo na kuonya dhidi ya kuwalenga maafisa wa polisi, akiahidi kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika.
Pia aliwataka maafisa hao kutumia silaha zao kuwalinda wao wenyewe na hata mali.
“Wakati mtu anakuja katika kituo cha polisi na anataka kuchukua ofisi ya serikali, bunduki ya polisi na maisha yako, mpige risasi,” Murkomen aliwaambia maafisa wa polisi.