logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Serikali Yaondoa Maafisa wa Polisi Waliokuwa Wakimlinda Babu Owino

Aliwahimiza wananchi kubaki waangalifu na kushikamana, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwajibika kwa wananchi na si kuwatishia wanaowaunga mkono.

image
na Tony Mballa

Habari26 June 2025 - 09:58

Muhtasari


  • Mbunge huyo alishiriki maandamano ya amani kupigania haki za wananchi dhidi ya kile alichokitaja kuwa ni kushindwa kwa serikali kuwajibika.
  • Anaona hatua ya kuondolewa kwa ulinzi wake kama kisasi kwa kutumia haki yake ya kidemokrasia.

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, amekosoa serikali kwa kumuondolea ulinzi kufuatia kushiriki kwake katika maandamano, akilitaja jambo hilo kuwa shambulio dhidi ya demokrasia.

Mbunge huyo alishiriki maandamano ya amani kupigania haki za wananchi dhidi ya kile alichokitaja kuwa ni kushindwa kwa serikali kuwajibika.

Anaona hatua ya kuondolewa kwa ulinzi wake kama kisasi kwa kutumia haki yake ya kidemokrasia.

“Jana nilisimama na wananchi, si dhidi ya taifa, bali kwa ajili ya mustakabali wake. Nilitumia haki yangu ya kidemokrasia kupinga kwa amani matendo ya serikali inayowatelekeza raia wake. Leo, kama kisasi, serikali imeondoa ulinzi wangu rasmi,” alisema Babu.

Babu Owino

“Wacha niseme wazi: hili si shambulio tu dhidi yangu, bali ni shambulio dhidi ya demokrasia yenyewe. Wakati wawakilishi waliochaguliwa wanaadhibiwa kwa kusimama na wananchi, ni ishara ya serikali inayohofia uwajibikaji, si serikali inayotumikia wananchi wake,” aliongeza.

Babu alieleza kuwa kuwaadhibu viongozi walioko madarakani kwa kuungana na raia kunadhoofisha demokrasia na kuonyesha kwamba serikali inaogopa kuwajibika. Alisisitiza kuwa ataendelea kutoa sauti kwa ajili ya haki licha ya vitisho vinavyolenga kumnyamazisha.

“Siogopi vitisho. Sitanyamazishwa. Sauti yangu, na sauti ya kila raia anayedai haki, usawa, na uhuru, zitazidi kusikika. Wakenya ndio ulinzi wangu,” alisema.

Aliwahimiza wananchi kubaki waangalifu na kushikamana, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwajibika kwa wananchi na si kuwatishia wanaowaunga mkono.

Babu Owino

“Kwa wananchi: kaeni chonjo, kaeni pamoja, na mjue kuwa viongozi wenu wanapaswa kuwajibika kwenu, si kuwatishia wale wanaosimama nanyi. Ukweli hauwezi kufichwa. Harakati za kutafuta haki haziwezi kuzuiwa,” aliongeza.

Anaamini kuwa ukweli na harakati za kudai haki haviwezi kusitishwa, akisisitiza tena kuunga mkono madai ya wananchi ya usawa na uhuru.

Mbunge huyo siku ya Jumatatu alitimiza ahadi yake kwa kujiunga na waandamanaji wengine jijini Nairobi katika maandamano ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha ambayo yaligharimu maisha ya watu wasiopungua 60.

Babu siku ya Jumanne aliwahimiza vijana kuendelea kupigania haki kwa heshima ya kizazi cha Gen Z kilichopoteza maisha mnamo Juni 25, 2024, wakati wa maandamano hayo.

"Nachoweza kuwaambia kaka na dada zangu wa Gen Z ni kupambana, songeni mbele. Haijaisha hadi iishe," Babu alisema.

"Mengi yanaweza kusemwa, mengi yanaweza kufanyika, lakini nawahimiza, niko nanyi. Katika kipimo cha sifuri hadi 10, niko nanyi kwa kiwango cha 11, naunga mkono kwa asilimia 101. Fanyeni, tufurahisheni, tuko pamoja, ninaunga mkono," aliongeza.

Babu Owino

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved