
Mahakama Kuu imeamuru Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kumwasilisha mwanablogu Ndiagui Kiangui mahakamani, ambaye ametoweka kwa siku 10.
IG anatarajiwa kumfikisha Ndiagui mahakamani bila kukosa au kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu ni kwa nini hawezi kupatikana.
“Hii ni ombi la habeas corpus linalomhusu Mkenya ambaye ni binadamu… Nimezingatia ukweli kwamba mlalamikaji wa pili hajapatikana kwa siku 10 na maisha ya raia yamo hatarini,” alisema Jaji Chacha Mwita.
Mahakama iliagiza kuwa ombi hilo liwasilishwe kwa walalamikiwa kabla ya mwisho wa siku ya kazi ya Jumatatu, huku majibu yakitarajiwa ndani ya siku saba.
Katika uamuzi wa moja kwa moja, Jaji Mwita aliamuru IG ama amlete Kiangui mahakamani au atoe maelezo ya kuridhisha kufikia Jumanne saa 5:00 asubuhi wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo.
Ombi hilo liliwasilishwa baada ya kutopatikana kwa Kiangui kwa zaidi ya juma moja, hali iliyoibua hofu kuhusu uwezekano wa kutoweshwa kwa kulazimishwa.
Maendeleo haya yanajiri siku chache tu baada ya Amnesty Kenya kudai kuachiliwa kwa mwanablogu huyo ambaye hajulikani aliko tangu Jumamosi, Juni 21, kufuatia taarifa ya kuvamiwa kwake nyumbani katika mtaa wa Kinoo.
Amnesty Kenya ilihusisha kutoweka kwake na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Walidai aachiliwe huru au afikishwe mahakamani, badala ya kuzuiliwa kwa siri bila mawasiliano yoyote.
“Achilieni huru Ndiangui Kinyagia. Mara ya mwisho alionekana Juni 21 baada ya uvamizi wa maafisa wa DCI nyumbani kwake Kinoo. Tunataka aachiliwe mara moja. Ikiwa anatuhumiwa kwa kosa lolote, afikishwe mahakamani — si kuzuiliwa kwa siri,” Amnesty ilidai.
Kulingana na familia, Kinyagia, mtaalamu wa TEHAMA mwenye umri wa miaka 31 na mchambuzi maarufu mtandaoni, alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kundi la wanaume wanaoaminika kuwa maafisa wa DCI kuzingira jengo lake la makazi huko Kinoo.
Mashahidi walisema maafisa hao walifika kwa magari kadhaa yasiyo na alama za utambulisho na walikaa nje ya jengo hilo kwa takriban saa tisa kabla ya kuivamia nyumba yake kwa nguvu.
Kwa mujibu wa familia, waliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha Kinoo, lakini maafisa walikana kuhusika na operesheni hiyo au kujua aliko Kinyagia.
Kinyagia ndiye kijana aliyehusika na ratiba ya maandamano ya Jumatano, Juni 25, ambayo iliweka wazi mfululizo wa matukio ya maandamano hayo kuanzia mwanzo hadi mwisho. Hata hivyo, licha ya kuweka ratiba hiyo, Kinyagia hakuhudhuria maandamano hayo na hajulikani aliko tangu alipotekwa kwa nguvu.