
Waziri wa Afya Aden Duale amemfokea vikali aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kutokana na matamshi yake ambayo alidai yanaweza kuchochea ghasia.
Akizungumza wakati wa mazishi ya shangazi yake wa mwisho aliyekuwa hai, Gladys Gathoni Kahua, Gachagua alidai kuwa jamii yake ya Wakikuyu inalengwa kufuatia mvutano wake na serikali ya Kenya Kwanza.
“Kama jamii, tuko matatani na kwenye njia panda,” alisema.
“Sijali kuhusu mimi binafsi kwa sababu mimi ndiye niliyesababisha haya yote, hivyo naweza kuteswa na hata watoto wangu wakaumia, lakini kwa jamii yangu, tunahitaji msaada.”
Aliyekuwa Naibu Rais aliondolewa madarakani kupitia kura ya bunge mwezi Oktoba 2024 kufuatia mvutano mkali na Rais William Ruto.
Tangu wakati huo, ameunda chama chake kipya—Democracy for the Citizens Party (DCP)—chini ya kaulimbiu Skiza Wakenya.
Chama hicho kilizinduliwa Mei 15 katika eneo la Lavington, Nairobi, ikiwa ni sehemu ya mpango mkuu wa Gachagua wa kumng’oa Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Katika majibu yake yaliyojaa ukali, Duale alilaani matamshi ya Gachagua akiyaita kuwa ni ya “uzembe” na “hatari”.
“Tunajua Bwana Gachagua yuko katika hali ya kujiharibu. Lakini hawezi kuiteketeza nchi anapojiharibu mwenyewe. Kauli kama hizi zisizo na busara ni hatari kwa amani na uthabiti wa taifa letu. Hii ni kudhalilisha viwango vya uongozi,” alisema Waziri huyo.
Gachagua katika wiki za hivi karibuni amekuwa akiongeza mashambulizi dhidi ya Rais Ruto, akiahidi kuhakikisha kuwa anakuwa kiongozi wa muhula mmoja tu.
Kama sehemu ya mkakati wake mkuu wa kumrejesha nyumbani bosi wake wa zamani, ameanza ziara ya kitaifa kutafuta uungwaji mkono, ya hivi karibuni ikiwa ni ziara ya siku mbili katika eneo la Magharibi mwa Kenya.
Alifuatana na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na viongozi wengine wa upinzani katika juhudi za kuvutia kura za jamii ya Waluhya, jumuiya inayokadiriwa kuwa na wapiga kura milioni 2.6, ikiwa ni ya pili kwa idadi baada ya Kati mwa Kenya.
Upinzani ulioungana unalenga kulitwaa eneo la Magharibi kutoka kwa Rais Ruto na mshirika wake mpya wa kisiasa, Raila Odinga, kabla ya uchaguzi mkuu.
“Nataka kuchukua fursa hii kuwashukuru watu wa taifa la Mulembe kwa uvumilivu wenu na upendo. Tumeawasikia kwa sauti kubwa na wazi, na nataka kuwahakikishia kuwa hatutasalimu amri wala kuwaangusha,” Gachagua alisema mwishoni mwa ziara hiyo siku ya Ijumaa.