
Rais William Ruto, Jumapili, alieleza kilichomchochea kujenga kanisa jipya kabisa ndani ya eneo la Ikulu jijini Nairobi.
“Ikiwa ninaishi kwenye nyumba ya mawe katika Ikulu, halafu hapo hapo kuna kanisa la mabati, nitamwambia nini Mungu siku tutakapokutana?” Ruto aliuliza.
Rais pia alikanusha madai kuwa kanisa linalojengwa Ikulu linagharimu Shilingi bilioni 1.2, kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la humu nchini.
Akizungumza wakati wa sherehe ya Maadhimisho ya Miaka 35 ya Dayosisi ya ACK ya Embu iliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kigari, Embu, Ruto alisema hajui chanzo cha takwimu hiyo.
Alisisitiza kuwa haiwezekani kwa kanisa hilo kugharimu zaidi ya jengo la ghorofa kumi na moja linalogharimu Shilingi milioni 350.
Rais alionya dhidi ya kusambaza propaganda na chuki dhidi ya kanisa la Mungu.
“Askofu amenionyesha jengo tunalojenga; lina ghorofa kumi na moja. Imekadiriwa kugharimu Shilingi milioni 350. Hebu niwaulize: kama kanisa linaweza kubeba watu 300, kweli linaweza kugharimu bilioni moja? Tafadhali acheni porojo, propaganda na chuki. Kwa nini mnalichukia kanisa la Mungu? Sijui walipozipata hizo bilioni,” alisema Ruto.
Aliendelea kueleza kuwa kanisa hilo litahudumia familia takriban 300 za wafanyakazi walioko Nairobi.
Ruto alifafanua kuwa hakulianzisha kanisa hilo, bali alilikuta likiwa tayari, na alichofanya ni kulibadilisha kutoka kuwa la mabati hadi kuwa la kudumu.
“Kanisa tunalojenga ni kubwa vya kutosha kwa ajili ya watoto na familia 300. Tuna shule ya Jumapili pale. Sikulianzisha kanisa; nililikuta. Nimefanya tu uamuzi kwamba badala ya kuwa la mabati, tulijenge kwa mawe.”
Ruto alisema wanaosambaza taarifa hizo wana njama ya kuipinga serikali.
“Wamepanga mengi kutupinga na kutudharau. Naomba mheshimu neno la Mungu. Wale walioko Ikulu ni Wakenya kama wengine na pia ni Wakristo.”
Rais alisema hawezi kuendelea kuchanga pesa kujenga makanisa kote nchini ilhali lile la Ikulu linabaki kuwa la mabati.
Alihoji jinsi anaweza kukarabati Ikulu na kuishi mahali pazuri ilhali kanisa la Mungu linabaki kwenye jengo la mabati.