
Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi amemwambia kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua asahau kabisa nia yake ya kuingia uongozini kwa njia za mkato.
Akizungumza katika Kaunti ya Migori siku ya Jumapili, Wandayi aliwataka Gachagua na viongozi wenzake wa upinzani kusubiri uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Wandayi alidai kuwa maandamano ya kizazi cha Gen Z yanachochewa na viongozi wa upinzani wakiongozwa na Gachagua, akisema kuwa mpango wao wa kutaka kutwaa madaraka kwa njia isiyo ya kikatiba hautafaulu, na hivyo wanapaswa kuwa na subira hadi uchaguzi mkuu ujao.
“Maandamano hayakuongozwa na vijana, bali na viongozi wenye tamaa ya madaraka. Wanajificha nyuma ya watoto wa watu wengine. Tunawaonya waache tabia hiyo. Wasubiri uchaguzi ujao,” alisema Wandayi.
Waziri huyo aliwasihi wakosoaji wa serikali ya Kenya Kwanza kuwa wavumilivu hadi mwaka wa 2027, akieleza kuwa kwa sasa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeundwa kikamilifu na iko tayari kusimamia uchaguzi huru na wa haki.
Kauli ya Wandayi iliungwa mkono na Mbunge wa South Mugirango, Silvanus Osoro, ambaye alisema kuwa wanaunga mkono juhudi za mazungumzo ya kitaifa zinazoongozwa na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.
Osoro alisema kuwa viongozi wasiopenda kushiriki katika mazungumzo wanapaswa kutoa nafasi kwa Wakenya wanaotaka kushiriki kwenye majadiliano hayo.
Aidha, mbunge huyo alimshauri Gachagua kuacha kumshambulia Raila Odinga, akisisitiza kuwa si wa kiwango kimoja naye kisiasa.
Haya yanajiri huku viongozi mbalimbali wanaomuunga mkono Rais William Ruto wakiwataka viongozi wa upinzani waache kufikiria kuwa wanaweza kuingia mamlakani kwa njia za mkato au za kupindua serikali.