
Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetang'ula, amemsifu Rais William Ruto kwa kuwaajiri walimu wapya 76,000 katika kipindi kifupi tangu aingie madarakani.
Akizungumza katika eneo la Igembe Kaskazini, Kaunti ya Meru, Wetangula alisema ajira hizo za hivi karibuni ni uthibitisho kuwa serikali ya sasa inatilia mkazo sekta ya elimu.
Kulingana naye, walimu wengine 24,000 wanatarajiwa kuongezwa kwenye orodha ya malipo ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) katika mwaka huu wa fedha, hatua itakayofikisha jumla ya walimu 100,000 walioajiriwa ndani ya miaka mitatu ya utawala wa sasa.
“Tangu Rais Ruto aingie madarakani, ni kweli kwamba ameajiri walimu 76,000 katika kipindi cha miaka miwili. Katika bajeti ya sasa, tumeweka fedha za kuwaajiri walimu wengine 24,000 ili tufikishe jumla ya walimu 100,000 ndani ya miaka mitatu,” alisema Wetangula.
“Jambo kama hili halijawahi kushuhudiwa nchini tangu kupata uhuru,” aliongeza.
Wetangula alisisitiza kauli kama hiyo iliyotolewa na Rais William Ruto, ambaye alifichua kuwa walimu hao wapya wanaweza kuajiriwa kufikia Januari 2026 ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa walimu unaosababisha upungufu wa wafanyakazi katika shule nyingi nchini.
Hata hivyo, Rais Ruto alibainisha kuwa changamoto za bajeti zimepunguza idadi ya walimu wanaoajiriwa katika kila awamu ya ajira, licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya walimu waliobobea lakini hawana ajira.
“Wakenya waliniomba nitatue changamoto katika sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na matatizo yanayoathiri mpito wa Mtaala wa Umahiri (CBC). Tumekuwa na changamoto za upungufu wa walimu, ukosefu wa miundombinu ya shule, huku vyuo vikuu vikikosa fedha,” alisema Ruto.
Katika bajeti iliyoidhinishwa ya mwaka wa fedha 2025/2026, TSC imetengewa Sh387 bilioni, ambapo Sh7.2 bilioni zimepangiwa kuajiri walimu wa mkataba (interns).