
Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amemshutumu kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa unafiki kuhusu pendekezo lake la kuanzisha mazungumzo baina ya vizazi kwa lengo la kuleta maelewano kati ya serikali na vijana wa taifa.
Akizungumza katika eneo la Kilome baada ya kuhudhuria uzinduzi wa kituo cha afya cha Maria Salus huko Kiongwani, Kaunti ya Makueni, Kalonzo aliwataka Raila na mshirika wake wa kisiasa, Rais William Ruto, kushughulikia moja kwa moja masuala yaliyotolewa na kizazi cha Gen Z cha Kenya.
Alisema mapendekezo yaliyotolewa na mshirika wake wa zamani wa kisiasa hayatatatua changamoto zinazoikabili nchi, akisisitiza kuwa vijana wa Kenya tayari wamezungumza kwa sauti na wazi, na sasa ni wakati wa kuchukua hatua
“Rafiki yangu Raila alisema ooh, tufanye intergenerational dialogue. Hawa watoto hawataki mazungumzo. Wanataka elimu ya chuo kikuu na ufadhili wa maana; wanataka kufikia vyuo vya elimu ya juu. Wale walio katika viwango vya chini wanataka elimu ya msingi bila malipo,” alisema Kalonzo.
Akiwa mmoja wa waliohusika katika mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) na Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa (NADCO), Kalonzo alisema hataki kuona muda wa Wakenya ukipotezwa tena kwa mikutano ya mazungumzo ambayo, kwa maoni yake, hunufaisha watu wachache tu.
“Wakenya wanaomboleza, hatuwezi kuvumilia. Hatutaki mazungumzo yoyote na Ruto. Hatutaki. Hatutaki hayo mazungumzo. Mazungumzo ya kufanya nini? Tunataka haki chini ya Katiba,” alisisitiza Kalonzo.
Agizo la Rais Ruto la kuamuru waandamanaji kupigwa risasi miguuni, lililotolewa siku nane zilizopita, pia lililaaniwa vikali.
“Yeye amesema ‘enough is enough’ na watoto wapigwe miguu risasi. Hakuna rais mwingine, hata wale madikteta wakatili zaidi, waliwahi kutoa agizo kama hilo. Ati watu wapigwe miguu risasi waende hospitali, na hiyo hospitali yenyewe haifanyi kazi,” Kalonzo alisema.
Wakili Ndegwa Njiru aliongeza: “Hatutaruhusu serikali inayowaua watoto wetu. Hatutakubali mazungumzo yanayoitishwa na Raila. Hatutafanya mazungumzo na wauaji wetu. Watoto hawa wanahitaji matumaini.”