
Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga amezindua jukwaa la kidijitali la kuchangisha fedha kwa ajili ya kampeni yake ya urais mwaka 2027, akilitaja kuwa ni juhudi zinazoongozwa na wananchi kwa lengo la “Kurekebisha, Kurejesha na Kujenga upya Kenya.”
Tovuti hiyo, davidmaraga.com, inawawezesha Wakenya kuchangia kuanzia Shilingi 50 ili kuunga mkono azma yake ya kuwania urais.
Maraga alieleza kuwa ndani ya siku mbili, michango kutoka kwa Wakenya walioko nchini ilizidi Shilingi 500,000, huku michango ya ziada ikitoka kwa Wakenya waishio ughaibuni kwa sarafu za kigeni.
“Tumeanzisha tovuti, davidmaraga.com, na ndani ya siku mbili hapa nchini, tulipata zaidi ya Shilingi 500,000. Wale waishio diaspora pia wamechangia kwa dola. Hii inaonyesha kuwa Wakenya wanataka mabadiliko,” alisema.
Jaji huyo mstaafu alisisitiza kuwa atategemea zaidi msaada kutoka kwa umma kufadhili kampeni zake, akisema mchango wake binafsi utakuwa wa kiwango cha chini.
“Nitawaomba Wakenya wachangie kampeni hizi. Mimi nitaweka fedha kidogo sana, kama Shilingi milioni moja au mbili. Sina pesa nyingi,” alisema katika mahojiano na Citizen TV.
Jukwaa hilo linawataka wachangiaji kuwasilisha majina yao, nambari ya simu, anwani ya barua pepe, na kiasi wanachotaka kuchangia.
Kwa mujibu wa Maraga, fedha hizo zitatumika kwa uhamasishaji mashinani, mikutano ya miji, uenezaji wa taarifa kidijitali, na uundaji wa mtandao wa kitaifa wa wajitoleaji.
Aliwahakikishia wachangiaji kuwa kila senti itahesabiwa, na kiasi chochote kitakachosalia kitaelekezwa kwa manufaa ya umma.
“Kwa mateso ambayo Wakenya wamepitia, nina hakika tutapata Shilingi 50 au 100 kutoka kwa mtu mmoja mmoja. Natumai tutapata ziada, na chochote kitakachosalia tutakitumia kwa shughuli ya kijamii,” alisema.
Maraga alisisitiza maono yake ya kuunda serikali inayoongozwa na wataalamu na watu wenye ujuzi, akieleza kuwa nyadhifa serikalini zitatengewa wale tu wenye uwezo na uwajibikaji.
“Kila mtumishi wa umma lazima apate nafasi yake kwa stahili na atoe matokeo. Hatutakuwa na serikali ya zawadi na upendeleo,” alisema.