
NAIROBI, KENYA, Julai 24, 2025 –Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Ruto, amewajibu wakosoaji wake kwa kuwataka kuwasilisha mpango mbadala wenye mashiko badala ya kurudia kauli zenye hisia kama “Ruto Must Go”, “Kasongo” na “WanTam”.
Ruto awataka wakosoaji watoe hoja zenye msingi
Akizungumza kuhusu hali ya sasa ya kisiasa nchini, Rais Ruto alisema amewasikiliza Wakenya wanaopaza sauti wakitaka aondoke mamlakani, lakini akasisitiza kuwa kauli hizo haziwezi kuwa mbadala wa sera bora.
“Nimewasikiliza Wakenya wanaosema ‘Ruto must go’, ‘WanTam’, lakini ukweli ni kwamba muda wangu utafika na nitaondoka kama waliotangulia. Lakini je, sababu zenu ni zipi za kusema ‘Ruto must go’?” Rais Ruto aliuliza kwa uketo.
Kauli za kisiasa zapuuzwa kama si suluhisho la matatizo
Rais Ruto alionekana kuelekeza ujumbe wake kwa viongozi wa upinzani wanaotumia kauli maarufu za mitandaoni na mikutano ya hadhara kama njia ya kuhamasisha umma dhidi ya utawala wake.
Amesisitiza kuwa siasa za kupandikiza hisia bila mwelekeo wa sera zinaweza kudhoofisha taifa badala ya kulijenga.
“Tunahitaji mawazo yanayojengwa juu ya sera na si mihemko. Wale wanaosema ‘Ruto must go’, waambie Wakenya mpango wao ni upi wa maendeleo, ajira, au kupunguza gharama ya maisha,” alisema Ruto.
Ruto adokeza kuhusu urithi wake wa uongozi
Katika matamshi yaliyobeba uzito wa kiongozi anayefahamu muda wake wa kuondoka, Rais Ruto alikiri kuwa hatadumu milele madarakani, lakini akataka hoja zenye msingi ndizo zitumike kumhukumu.
“Mimi si wa kwanza kuwa Rais wa Kenya, na sitakuwa wa mwisho. Lakini tukiendelea kuchochewa kwa kauli tupu, basi hatutajenga taifa bali tutalibomoa,” Rais aliongeza.
Kauli zake zazua mjadala mpana
Kauli ya Rais imezua mjadala mpya katika ulingo wa siasa, huku baadhi ya wachanganuzi wakisema alilenga kupunguza mvutano unaoendelea mitaani, huku wengine wakitafsiri ujumbe huo kama changamoto kwa upinzani kuonyesha uwezo wa kiutawala.
Kwa sasa, mvutano wa kisiasa unaendelea kushika kasi huku upinzani ukiahidi maandamano zaidi, na serikali ikitoa wito wa mazungumzo yenye nia njema kwa mustakabali wa taifa.