
NAIROBI, KENYA, Julai 26, 2025 — Mshauri wa Rais William Ruto, Farouk Kibet, amemjibu kwa ukali aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akimtuhumu kwa kuchochea siasa za chuki baada ya kushindwa kuwajibika alipokuwa serikalini. Farouk pia ametoa changamoto kwa viongozi kuwekeza mashinani badala ya mijini pekee.
Katika hotuba kali aliyotoa Bungoma, Kibet alimshutumu aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, kwa kuendeleza siasa za chuki na kudhoofisha serikali aliyoitumikia. Farouk alimtaja Gachagua kuwa chanzo cha migawanyiko ya kikabila na kisiasa nchini, akisema kuwa kauli zake za hivi karibuni zina nia ya kuharibu mafanikio ya serikali ya Kenya Kwanza.
Farouk Amvaa Gachagua Bungoma
Akihutubia wakazi wa Kanduyi, Bungoma, wakati wa hafla ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, Farouk Kibet alimshutumu vikali Gachagua kwa kutumia jukwaa la kimataifa nchini Marekani kueneza taarifa za kupotosha kuhusu serikali.
“Hatutaruhusu viongozi waliokosa ufanisi wakiwa serikalini kutufundisha uongozi. Ulishindwa ukiwa Naibu Rais, sasa unatafuta huruma kwa kuchochea mgawanyiko,” alisema Farouk huku akishangiliwa na umati.
Aliongeza kuwa serikali ya Kenya Kwanza haifanyi kazi kwa misingi ya kikabila bali kwa kuzingatia maendeleo ya kila Mkenya.
“Sisi hatuamini kuwa Kenya ina ‘wenye hisa’ na ‘wasio na hisa’. Huo ni mtazamo potofu unaotugawa kama taifa. Tunaamini kila Mkenya ana haki sawa ya kufaidika na serikali yao,” alisisitiza.
Gachagua, ambaye sasa anaongoza chama kipya cha Democratic Change Party (DCP), alisema akiwa Marekani kwamba Farouk na mbunge mmoja wa Bonde la Ufa wanampotosha Rais kuhusu mgao wa fedha za shule. Alidai kuwa serikali imesaliti wananchi kwa kupunguza mgao wa capitation kwa shule za umma.
Mbadi: Bunge Lina Lawama, Si Serikali
Waziri wa Hazina ya Kitaifa, John Mbadi, alijitokeza pia kumjibu Gachagua, akifafanua kuwa kupunguzwa kwa fedha za elimu ni jukumu la Bunge, si la Farouk wala serikali kuu.
“Serikali ilipendekeza mgao wa Sh22,000 kwa kila mwanafunzi wa sekondari. Lakini Bunge, ambalo Gachagua alikuwa sehemu yake kabla ya kuwa Naibu Rais, likapunguza kiasi hicho hadi Sh17,000,” alisema Mbadi akiwa Suba South katika hafla ya shukrani.
“Tumepeleka fedha zote tulizoidhinishiwa kwenye bajeti. Kama hazitoshi, basi ni jukumu la Bunge kuongeza. Tuwache kugeuza bajeti kuwa silaha ya kisiasa,” Mbadi aliongeza.
Farouk Asema Siasa za Miji Zinaleta Uonevu Mashinani
Farouk aliwataka viongozi wanaotoa misaada yao mijini kuangalia upya mtazamo wao wa maendeleo.
“Wapo wanaojitokeza Nairobi kutoa misaada na kupiga picha, lakini mashinani hakuna chochote. Huo si uongozi, ni kujitafutia umaarufu,” alisema.
Akitetea sera ya bottom-up, Farouk alisema kuwa serikali inalenga kushughulikia matatizo ya kiuchumi kwa kuanzia mashinani.
“Tunafanya kazi ya kweli. Tunaweka pesa kwenye makundi ya kina mama, vijana na walemavu kwa sababu tunajua kuwa ukimwezesha mwananchi wa kawaida, unaiokoa nchi nzima,” alieleza.
Alibainisha kuwa hafla hiyo ya Kanduyi ilichangisha fedha kusaidia zaidi ya vikundi 50 vya wanawake, na kuahidi kwamba serikali itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha uchumi wa mashinani unapaa.
Gachagua Aendelea Kujitenga na Serikali
Rigathi Gachagua, ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto kwenye uchaguzi wa 2022, ameanza kujitenga kisiasa na utawala wa Kenya Kwanza. Amejibandika lebo ya "mtetezi wa Mlima Kenya", huku akieneza shutuma dhidi ya washirika wa zamani serikalini.