
“Tumesema kuwa maandamano yasitumike kuharibu mali ya watu. Tunataka maandamano yawe ya amani, yaeleze maoni kwa mujibu wa sheria na si kisingizio cha kuharibu mali ya Wakenya,” alisema Kibet.
Kauli yake ilitolewa siku chache baada ya kumshutumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuchochea maandamano ya hivi majuzi jijini Nairobi.
Maandamano hayo, ambayo yalilenga kushinikiza hatua kuchukuliwa kuhusu mauaji ya mwanablogu Albert Ojwang, yaliishia kuwa vurugu.
Polisi walitumia vitoa machozi na magari ya maji kuwatawanya waandamanaji hadi jioni.
Wakati wa maandamano hayo, mali iliharibiwa na magari mawili kuchomwa moto. Kibet alimtaka Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kuchukua hatua na “kulinda” jiji dhidi ya uharibifu huo.
Akijibu wito huo, Gavana Sakaja alisema wale waliohusika na uharibifu wa mali ya umma jijini Nairobi wakati wa maandamano watakamatwa.
Gavana huyo alisema kuwa uchunguzi wa kina utafanywa na wale watakaopatikana na hatia watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Sakaja alisisitiza kuwa katiba inaruhusu maandamano ya amani lakini si ya fujo, na kuwataka Wakenya, hususan wanasiasa, kuepuka siasa za mgawanyiko.
Maandamano hayo yalifuatia mauaji ya Ojwang, ambaye alifariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi Jumapili.
Uchunguzi kuhusu kifo cha Ojwang katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Nairobi unaendelea, huku maafisa wa polisi waliokuwa kazini kituoni humo wakisimamishwa kazi.
Maafisa wa polisi, akiwemo OCS wa Kituo Kikuu cha Polisi Samson Talaam na James Mukhwana, wamekamatwa.
Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) inaendelea na uchunguzi kuhusu suala hilo.