
NAIROBI, KENYA, Julai 27, 2025 — Rais William Ruto ametoa wito kwa Wakenya kumruhusu kutumikia mihula miwili ilivyo kikatiba, akisema kwamba ni kwa njia hiyo tu ndoto ya Kenya yenye maendeleo itatimia.
Rais alizungumza katika eneo la Kariobangi Jumapili baada ya kuhudhuria Ibada ya Kanisa la ACK St Martins Light Industries, ambapo alisimama kuzungumza na wananchi waliofika kumsikiliza.
“Nasikia mnasema mihula miwili, lakini sikilizeni, hiyo mihula miwili ni ya maendeleo. Ni ya makazi nafuu, kujenga masoko, kupanga elimu, kuweka mpango wa Afya ya Jamii ili kila Mkenya apate huduma,” alisema Rais Ruto.

Ruto alikosoa mjadala wa “Ruto lazima aondoke,” akisema kuwa wanaoendeleza hoja hiyo hawana mpango mbadala wa maendeleo.
“Kama ni ‘Ruto lazima aende’, basi niambie nitaenda vipi. Una maana gani unaposema Ruto lazima aondoke? Leta mpango bora umshawishi Mkenya. Huwezi kuondoa mpango usiokupendeza bila kuwa na mpango mwingine,” alisema kwa msisitizo.
Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula aliwahimiza Wakenya kumchagua tena Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027, akisema kuwa uongozi wake umedhihirisha dhamira ya kweli ya maendeleo.
“Naomba watu wa Meru waunge mkono Serikali ya Rais Ruto kwa dhati kwa sababu anastahili muhula wa pili kwa rekodi yake ya maendeleo,” alisema Wetang’ula.
Rais Ruto alisisitiza kuwa mafanikio ya taifa hayawezi kupatikana kwa mabadiliko ya uongozi kila baada ya kipindi kimoja.
“Suluhu ya changamoto zetu haipatikani kwa mihula. Inapatikana kwa mikakati na mpango,” alieleza.