logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ukraine Yamkamata Mwanariadha wa Kenya Akipigania Urusi Vitani

Evans afichua namna Waafrika wanavyolaghaiwa kuingia vitani Russia.

image
na BRIAN ORUTA

Habari19 September 2025 - 08:28

Muhtasari


  • Mwanariadha Mkenya Evans amekamatwa na jeshi la Ukraine baada ya kudanganywa kujiunga na jeshi la Russia.
  • Asema alikwenda Russia kama mtalii, akaingizwa mtegoni, na sasa anataka kurudi Kenya kwa binti yake wa miaka 16.

Mwanariadha mmoja wa Kenya anayejulikana tu kama Evans amekamatwa nchini Ukraine akipigania upande wa Russia, baada ya kujisalimisha kwa Kikosi cha Piyade cha Ukraine karibu na mji wa Vovchansk katika mkoa wa Kharkiv Oblast.

Katika mahojiano ya video baada ya kukamatwa, Evans alieleza kuwa alisafiri hadi Urusi kama mtalii lakini akadanganywa na mpangaji wake hadi akaingizwa jeshini bila hiari.

“Nilijiunga na jeshi la Russia bila kujua kwamba nilikuwa narekodiwa. Sijawahi kuwa mwanajeshi wala kutaka kazi ya kijeshi. Nilikuja kama mtalii na nilikuwa nimetumia wiki mbili, lakini siku moja kabla ya kurudi, yule mtu aliyenipokea aliniuliza kuhusu Russia na nikasema ni nchi nzuri. Akaniuliza kama nataka kubaki, nikasema ndiyo, lakini visa yangu ilikuwa imeisha muda,” Evans alisema.

Mwanariadha wa Kenya (Evans) alikamatwa na askari wa Ukraine katika Mkoa wa Kharkiv, karibu na mji wa Vovchansk/SCREENGRAB

Alifichua kuwa mpangaji huyo aliahidi kumsaidia kurefusha visa na kumhakikishia kazi tayari. Hata hivyo, aliletwa nyaraka za Kirusi asizozijua, akasaini, na pasipoti pamoja na simu yake zikachukuliwa.

“Alikuja jioni na karatasi zilizoandikwa Kirusi, sikujua ni kazi ya kijeshi. Aliniambia nisaini na akachukua pasipoti yangu na simu, ndipo mambo yakaharibika,” aliongeza.

Baada ya kusaini, watu wengine walimchukua na kumsafirisha kwa masaa saba hadi kambi ya kijeshi. Kila alipojaribu kupinga, aliambiwa: “Ulishasaini nyaraka, huwezi kurudi nyuma. Hudumu au ufe.”

Evans alisema alipatiwa mafunzo ya wiki moja pekee kabla ya kutumwa mstari wa mbele, ambapo alikutana na wapiganaji wengine kutoka mataifa mbalimbali.

“Mimi si adui wa Ukraine. Nilijikuta katika hali isiyoepukika. Sikutambua nilichokuwa ninasaini—imetia doa maisha yangu,” alieleza kwa huzuni.

Baada ya kudondoshwa msituni, Evans alikimbia kwa siku mbili akitafuta jeshi la Ukraine.

“Naliondoa sare ya Kirusi na kukaa msituni kwa siku mbili nikitafuta wanajeshi wa Ukraine. Niliwafikia nikiwa nimeinua mikono, wakaniweka kifungoni, wakanipeleka kambini mwao, wakanipa chakula na maji. Wao ni watu wema. Russia wanaweza kudhani nimeshakufa,” alisema.

Evans, ambaye ni mzazi pekee wa binti mwenye umri wa miaka 16, anasema anataka tu kurejea nyumbani.

“Mimi ni mwanariadha, nimekuwa kwenye riadha zaidi ya miaka kumi. Sitaki Russia—nitakufa huko. Nina binti wa miaka 16 anayekaa na mama yangu. Ananihitaji,” alisema kwa hisia.

Kukamatwa kwa Evans kunakuja katikati ya ripoti kwamba Russia imekuwa ikiwalaghai Waafrika kwa ahadi za kazi na kisha kuwapeleka mafunzoni na baadaye vitani—madai ambayo Moscow imeendelea kukanusha.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved