NYERI, KENYA, Jumanne, Oktoba 22, 2025 – Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga amezua mjadala mkali baada ya kudai kuwa kifo cha Raila Odinga kilikuwa “mpango wa Mungu” wa kuokoa eneo la Mlima Kenya dhidi ya kile alichokiita ubaguzi na upendeleo wa kisiasa.
Akizungumza kwa lugha ya Kikuyu siku ya Jumanne, wakati wa mazishi mjini Nyeri, Kahiga alisema Mungu ndiye “aliingilia kati” kwa sababu “kulikuwa na mtafaruku mbinguni.”
“Mnaona vile mambo yalivyokuwa yamepangwa, lakini Mungu akaingilia kati,” alisema Kahiga. “Sasa kila mtu anaona kuna mkanganyiko. Hatukuwa na chuki na mtu yeyote, lakini Mungu alikuja kutupigania.”
Kahiga aliongeza kuwa ukaribu wa Raila na Rais William Ruto ulikuwa umefanya serikali kuelekeza miradi mingi katika eneo la Nyanza, na kuwacha maeneo mengine nyuma.
“Kwa wale ambao hawasafiri, nilikuwa kule,” alisema. “Baraka zote za serikali zilikuwa zinaenda huko kwa sababu ya mipango ya baadaye. Ilionekana kama sisi tulikuwa tumesahauliwa, lakini Mungu akaingilia na kubadilisha mambo.”
Gavana huyo pia alionekana kumtolea Rais kejeli, akisema Mungu “alisawazisha uwanja wa siasa” nchini.
“Sasa kila mtu amerudi kupanga upya,” alisema. “Mpango ulikuwa wa kutuondoa, lakini Mungu ni nani? Anakula ugali kwa mtu au analala Kayole?”
Alimaliza kwa kusema kuwa Mungu alimchukua Raila ili “kutuliza hali” mbinguni.
“Alikuja kwa njia yake,” alisema Kahiga. “Aliangalia akaona kuna mabishano mengi huko juu, ndipo akamchukua Baba akasaidie kutuliza mambo.”
Kauli hizi zimeenea sana mitandaoni na zimekosolewa vikali na viongozi kutoka pande zote za siasa.
Wengi wamesema maneno hayo hayana utu na hayafai kutolewa wakati taifa bado linaomboleza kifo cha Raila, kiongozi aliyeheshimika kwa kupigania demokrasia na haki nchini Kenya.
Baadhi ya viongozi wamemtaka Kahiga aombe radhi hadharani, wakisema maneno yake yanaweza kuongeza mgawanyiko nchini na kudhalilisha kumbukumbu ya kiongozi huyo mashuhuri.