
Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mkewe Susan Wangari wamehukumiwa kifungo cha miaka 12 na mwaka mmoja jela mtawalia baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi kuhusiana na zabuni ya barabara ya shilingi milioni 588.
Kesi hiyo ambayo imekuwa ikiendelea kusikilizwa kwa zaidi ya miaka mitano kufikia sasa hatimae imeamuliwa.
Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani ya ufisadi Thomas Nzioki siku ya Alhamisi, Februari 13 alimhukumu Waititu kifungo cha miaka 12 jela au kulipa faini ya shilingi milioni 53.5.
Zabuni hiyo ya yenye thamani ya shilingi 588,198,328 iliyohusisha ukarabati wa barabara kadhaa katika kaunti ya Kiambu, Thika, Limuru, Gatundu Kaskazini, Juja na Ruiru ilitolewa na serikali ya kaunti mnamo Februari 2018 kwa kampuni ya Testimony Enterprises Ltd.
Aliyekuwa waziri wa Barabara Kaunti ya Kiambu Luka Mwangi Wahinya, na mfanyabiashara Charles Mbuthia Chege pamoja na mkewe Beth Wangechi pia walipatikana na hatia ya njama ya ufisadi ya kuilaghai serikali ya kaunti ya Kiambu mamilioni ya pesa.
Siku ya Jumatano, Jaji Nzioki alitoa hukumu hiyo ambayo ilihitimisha malumbano ya kisheria ya miaka mitano baina ya washukiwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Mkewe Waititu kwa upande wake alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya shilingi 500,000.
Hakimu Nzioki akitoa hukumu hiyo alipuuzilia mbali tetesi za Waititu kwamba kesi hiyo ilichochewa kisiasa na utawala uliopita wa Jubilee kutokana na uhusiana wake na Rais William Ruto wakati huo akiwa naibu wa rais.
Badala yake, hakimu alithibitisha kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha kesi ya kulazimisha, iliyoungwa mkono na mashahidi 32 na vipande 129 vya ushahidi wa maandishi, ambao ulithibitisha hatia ya mshtakiwa bila shaka yoyote.
Baada ya kutathmini kwa makini ushahidi uliowasilishwa na pande zote na kwa kuzingatia kwa makini maoni, nina uhakika zaidi ya shaka yoyote kwamba upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya watuhumiwa," Nzioki alieleza baada ya kuamua kesi hiyo
Hakimu Nzioki alimpata Waititu na hatia ya makosa manne kwa kutoa zabuni ya KSh588 milioni bila kufuata utaratibu.
"Baada ya kutathmini kwa makini ushahidi uliowasilishwa na pande zote na kwa kuzingatia kwa umakini maoni, nina uhakika zaidi kwamba upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya watuhumiwa, Nzioki alisisitiza.